Highlands FM

Madereva bajaji wanawake wadai kufanyiwa ukatili

19 February 2024, 11:07

Na Mwanaisha Makumbuli, Mbeya

Madereva bajaji wanawake katika halmashauri ya jiji la Mbeya  wamelalamika kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na baadhi ya wanaume ikiwemo kutolewa lugha za fedheha na matusi, kitendo kinachowakatisha tamaa na kujiona hawastahili kufanya shughuli hiyo.

Halmashauri ya jiji la Mbeya imetajwa kuwa na zaidi ya bajaji 3447, huku kati ya hizo 11 zikiendeshwa na wanawake.

Akizungumzia changamoto hiyo kwa niaba ya wenzake kumi na moja (11), Neema Emmanuel amesema amefanya shughuli hiyo kwa zaidi ya miaka saba (7) na ndio anayoitegemea kumuingizia kipato kwa ajili ya kuwatunza watoto wake.

Kwa mujibu wa Neema changamoto kubwa wanazokumbana nazo wanawake wakiwa barabarani ni pamoja na kutolewa lugha za fedheha, kudharauliwa na kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo kutukanwa matusi kutokana na jinsia yao.

“tunavumilia tu lakini tunapitia changamoto kubwa sana tukiwa barabarani unakuta mtu anakutukana na wewe demu vipi na matusi mengine makubwa (aliyataja), hatukati tamaa huku ndiko tunakopatia mkate wa kila siku’

‘’Wakati mwingine unakutana na mtu anakutongoza ukimkatalia anakutukana na matusi ya nguoni, tunaomba serikali iendelee kutoa elimu kwa abiria na wananchi kwa ujumla wataumbue kuwa na sisi wanawake tuna haki sawa ya kufanya shughuli kama wanaume hivyo, tuendelee kuheshimiana’’

Neema ambaye ni mama wa watoto watatu amesema alijitosa kuingia kwenye kazi hiyo baada ya kumwona mwanamke mwenzake anaendesha bajaji, hivyo na yeye aliona kuwa sekta hiyo ina fursa kwa vijana wakiwemo wanawake.

Amesema kila mara alipokuwa akisafiri kwa kutumia bajaji alikuwa anaketi nafasi ya mbele ili ajifunze namna dereva anavyoendesha pamoja na kupangilia gia, jambo lililomrahisishia kujifunza na kuelewa haraka namna ya kundesha chombo hicho.

‘’Walionipa moyo ni baadhi ya madereva wenzangu wa kiume, kwani kuna watu walikuwa wakiniambia kuwa wewe mwanamke unafanya nini huko si uende nyumbani ukalee watoto wako, lakini sikukata tama hata kidogo ndio maana hadi leo ninafanya hii kazi’’ alisema

Jeremia Mwaitege ambaye ni dereva bajaji ameungana na Neema, akieleza kuwa mara nyingi akiwa barabarani amekuwa akishuhudia namna watumiaji wengine wa barabara wakiwemo madereva wanavyowanyanyapaa madereva wa kike.

Hata hivyo amempongeza Neema kutokana na maamuzi yake ya kuendelea kufanya shughuli hiyo licha ya changamoto anazokumbana nazo, akiwasihi watu kuelewa kuwa kazi hiyo sio ya wanaume peke yao bali hata wanawake wenye sifa wanaweza kuimudu kama Neema na wenzake kumi.

 “kwa hali ya maisha jinsi ilivyo wanawake hawapaswi kuchagua kazi, tunawapongeza kwa kuamua kuona fursa kwenye bajaji, lakini kitu kingine wanawake ni watu wanaozingatia sana sheria za usalama barabarani hawaendeshi hovyo kama sisi wanaume ukitaka kuwa salama tumia bajaji inayoendeshwa na dereva mwanamke’’

“Hata ikitokea abiria amesahau mzigo kwenye bajaji anayoendeshwa mwanamke anakuwa na uhakika wa kuupata kwa kuwa wao ni waaminifu tofauti akisahau kwenye bajaji anayoendesha mwanaume’’ alisema Jeremia.

Braiton  Paulo ni abiria anayetumia usafiri wa bajaji kila siku kutokana na shughuli zake za hapa mjini, amekiri kuwa madereva wanawake wamekuwa na lugha nzuri pamoja na ukarimu ukipanda bajaji zao tofauti ukimkuta dereva wa kiume.

“kunautofauti kati ya dereva bajaji mwanaume na mwanaume kwanza unavyoingia kwenye bajaji kuna utofauti hutumia lugha nzuri ya kumkaribisha mteja ata ukimpa fedha  anavyorudisha anasema asante na hata wakiwa barabarani wanazingatia sheria za usalama barabarani’’ alisema

Mwenyekiti wa umoja wa madereva  bajaji na wamilika bajaji jijini Mbeya Lukasi Mwakyusa amesema sekta ya usafirishaji haina jinsia isipokua wanachozingatia ni vigezo vya usalama barabarani vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo amewapongeza wanawake walijitokeza na kuona fursa kwenye sekta hiyo lakini alionya kuwa ikiwa watafanyiwa vitendo visivyofaa na madereva wenzao ni vyema wakatoa taarifa kwenye uongozi ili hatua ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

 “sekta ya usafirishaji haina mwanamke wala mwanaume sekta ina madereva wenye vigezo vya udereva vitakutambulisha kama wewe ni dereva pasipokuangalia jinsia yako wala hakuna mgawanyo wa wanawake au wanaume wenye taaluma ya kuendesha vyombo husika pia wanatambulika kwa mijibu wa sheria kamana kwamba wawe na leseni ambayo inatolewa mamlaka husika lakini pia awe anazitambua sheria za usalama barabarani’’ alisema

Kiongozi huyo alisema kwa sasa sekta ya usafirishaji imechangamkiwa na wanawake ikiwemo kwenye malori na mabasi ya abiria, akiwatolea wito kutokata tama na kuchangamkia fursa hiyo kwa lengo la kujiingizia kipato na kuachana na utegemezi kwenye familia zao.

Mkurugenzi wa shirika la sauti ya mama afrika, Thabita bughali amesema uwepo wa wanawake kwenye sekta ya usafirishaji ni matunda ya elimu ya usawa wa kijinsia walioitoa wadau kwa jamii na inapaswa kulindwa ili kuwaheshimisha wanawake.

 “Kazi ni kazi ilimradi ni halali, mimi nimepanda sana bajaji ambazo wanaendesha wanawake uendeshaji wao uko makini sana tofauti na wanaume na utasafiri kwa usalama kwa amani niwatoe hofu wanaume kuwa wanawake wanaweza .”alisema Thabita

Mwisho…….