Highlands FM

TBL yajitosa kutunza mazingira

22 March 2024, 16:46

Meneja wa kiwanda cha TBL Mkoa wa Mbeya Emanuel sawe

Na Samwel Ndoni,Mbeya

Wakazi wa jiji la Mbeya wameshauriwa kupanda miti rafiki na maji ili kukabiliana na tishio la mabadiliko ya tabianchi ambayo yameendelea kuathiri mazingira na vyanzo vya maji nchini.

Wito huo umetolewa na Meneja wa kiwanda cha kuzalisha Bia (TBL) mkoa wa Mbeya, Emanuel Sawe wakati akiongoza zoezi la kupanda miti ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya maji duniani.

Kampuni ya TBL imeadhimisha siku ya maji duniani  kwa kupanda miti zaidi ya 400  katika eneo la kiwanda, chanzo cha maji cha Mwatezi kilichopo Uyole na mabwawa ya kuhifadhia maji taka eno la Kalobe jijini Mbeya.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo Sawe amesema kampuni hiyo ipo mstari wa mbele kushirikiana na wadau wengine katika kuhakikisha mazingira yanatunzwa na kuhifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha leo na baadae.

“Nitoe wito kwa wananchi hasa wanaoishi jirani na vyanzo vya maji kuendelea kutunza vyanzo hivyo ikiwemo kupanda miti rafiki na maji ili kuwezesha mvua kuendelea kuwepo muda wote, ukizingatia kuwa kwa sasa dunia ipo kwenye mapambano na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Sawe amesema kilichoisukuma kampuni hiyo kupanda miti ni athari ya mabadiliko ya tabianchi ambayo imesababisha ukame na ongezeko la joto katika maeneo mengi duniani pamoja na upungufu wa maji.

Hata hivyo ameiomba  serikali kuendelea kusimamia sheria za uhifadhi wa mazingira ikiwemo kudhibiti shughuli za binadamu jirani na vyanzo vya maji hususani kilimo, ufugaji na maendeleo ya makazi.

Kwa upande wake afisa uhusiano na huduma kwa wateja kutoka mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira jiji la Mbeya (UWSA), Neema Santoni ameishukuru kampuni ya TBL kwa kuwa mstari wa mbele kuhifadhi vyanzo vya maji.

‘’Niwapongeze TBL wamekuwa mstari wa mbele, kila mwaka tumekuwa tukishirikiana nao kupanda miti kwenye vyanzo vyetu vya maji, tunaendelea kuwaomba wakati mwingine wasichoke kuendelea kushirikiana nasi ili kwa pamoja tuweze kulinda vyanzo vyetu’’ alisema