Highlands FM
Highlands FM
6 October 2026, 8:53 am

Habari za watu wenye ulemavu zinahitaji sauti zaidi! Wandishi wahamasishwa kutumia kalamu zao kuibua haki, changamoto na mafanikio yao.
Na Samwel Mpogole
Wandishi wa habari kutoka redio jamii kumi za mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, wamehamasishwa kuongeza uandishi wa habari zinazohusu watu wenye ulemavu, kwa lengo la kuelimisha jamii, kupunguza unyanyapaa na kuibua haki, changamoto na mafanikio yao.
Hamasa hiyo imetolewa katika mafunzo yaliyofanyika jijini Mbeya, yaliyoandaliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Vyombo vya Habari Finland, VIKES, yakilenga kuwajengea waandishi uwezo wa kuandika habari za watu wenye ulemavu kwa kuzingatia utu, heshima na lugha sahihi.
Wandishi walioshiriki mafunzo hayo wamesema wamepata uelewa zaidi kuhusu namna ya kuibua na kuwasilisha habari za watu wenye ulemavu, huku wakieleza umuhimu wa kuongeza sauti zao kupitia vyombo vya habari.
Kwa upande wao, baadhi ya watu wenye ulemavu, akiwemo Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Mbeya, Evans Mwakyusa, wamesema waandishi wa habari ni wadau muhimu katika kuibua changamoto zinazowakabili.
Wamewataka waandishi kuongeza ziara katika maeneo ya vijijini ili kubaini changamoto za watu wenye ulemavu, kuzifikisha kwa jamii na mamlaka husika, pamoja na kuangazia fursa na mafanikio yao.
Wawezeshaji wamewataka waandishi kuangazia si changamoto pekee, bali pia haki, fursa, uwezo na mafanikio ya watu wenye ulemavu, ili habari ziwe chombo cha kuelimisha jamii na kupunguza mitazamo hasi
