Highlands FM
Highlands FM
19 November 2026, 4:08 pm

Ugumba umekuwa changamoto kwa wanawake wengi, ukisababisha matatizo ya kiuchumi, kisaikolojia na kijamii, yakiwemo unyanyapaa, migogoro ya ndoa na ukatili wa kijinsia.
Na Mwanaisha Makumbuli
Hali ya kutopata mtoto licha ya jitihada za kupata ujauzito imekuwa ikiwakabili wanawake wengi na kuwa chanzo cha changamoto mbalimbali za kiuchumi, kisaikolojia na kijamii, huku baadhi yao wakikumbana na unyanyapaa, kejeli, migogoro ya ndoa pamoja na ukatili wa kijinsia.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa takribani mtu mmoja kati ya sita duniani hukumbwa na tatizo la ugumba katika maisha yake, huku viwango vya tatizo hilo vikikadiriwa kuwa asilimia 17.8 katika nchi zenye kipato cha juu na asilimia 16.5 katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.
Tanzania, takwimu ulizokusanya zinaonesha kuwa ugumba wa awali unakadiriwa kuwa kati ya asilimia 1.8 hadi 2, huku ugumba wa pili ukikadiriwa kuwa kati ya asilimia 15.4 hadi 18.
Kwa wanawake wanaokumbwa na hali hiyo, gharama za vipimo, matibabu na safari za kutafuta huduma katika vituo mbalimbali vya afya zimekuwa mzigo mkubwa wa kifedha, hasa kwa wale wenye kipato cha chini.
Lakini zaidi ya changamoto hizo, wapo wanawake wanaopitia maumivu ya kihisia kutokana na kutopata watoto, huku wakikabiliwa na maneno ya kuudhi, lawama na shinikizo kutoka kwa familia na jamii.
Mbali na changamoto zinazowakabili wanawake hao, baadhi yao wamekuwa wakikabiliwa na migogoro ya ndoa, ikiwemo kufukuzwa katika familia, kupewa talaka au wenzi wao kuoa wanawake wengine kutokana na kutopata mtoto.
Hali hii inaibua umuhimu wa viongozi wa dini kutoa elimu na ushauri kwa waumini kuhusu namna ya kuwasaidia wanandoa wanaopitia changamoto za uzazi badala ya kuwahukumu au kuwabagua.
Aidha, changamoto hizi zinaweza kusababisha msongo wa mawazo, huzuni, kupoteza kujiamini na hata kujiona hawana thamani katika jamii.
Mwanasaikolojia CHRIS MZUBWE anaeleza athari za kisaikolojia zinazoweza kuwapata wanawake wenye matatizo ya ugumba na utasa, pamoja na umuhimu wa kuwapatia msaada wa kitaalamu ili waweze kukabiliana na hali hiyo.
Jamii inapaswa kuondoa dhana potofu zinazohusisha uwezo wa mwanamke kuzaa na thamani yake, huku familia, viongozi wa dini na wadau wa afya wakishirikiana kutoa elimu, msaada na ulinzi dhidi ya unyanyapaa na ukatili.
Kwa ujumla, changamoto ya kutopata mtoto si sababu ya kumdhalilisha mwanamke, bali ni suala la kiafya linalohitaji uelewa, upendo, msaada na heshima kutoka kwa jamii.