Highlands FM
Highlands FM
5 October 2026, 3:12 pm
Na Mwanaisha Makumbuli,Highlands Fm Radio
Katika miaka ya hivi karibuni, athari za mabadiliko ya tabianchi zimeanza kujidhihirisha kwa kasi kubwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya.
Wilaya hii, ambayo kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ina idadi ya wakazi takriban 344,471, kwa sasa inakabiliwa na ongezeko kubwa la joto, uhaba wa mvua, na kukauka kwa vyanzo vya maji. Hali hii inachochewa kwa kiasi kikubwa na shughuli za kibinadamu, hususan ukataji holela wa miti kwa ajili ya uzalishaji wa mkaa, kuni na mbao.
Hapa tunaangazia kwa kina ukubwa wa tatizo hili, athari zake katika sekta za kilimo na kijamii, pamoja na ushuhuda kutoka kwa wananchi na wataalamu mbalimbali.
Ukubwa wa Uharibifu wa Misitu
Takwimu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya zinaonesha picha ya kutisha. Kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka 2025, zaidi ya hekta 1,000 (sawa na hekari 2,500) za misitu zimepotea kutokana na uvunaji holela wa miti.
Zaidi ya hayo, kwa mujibu wa ripoti ya Global Forest Watch ya mwaka 2020, Chunya ilikuwa na hekta 870,000 za misitu, zilizofunika zaidi ya asilimia 50 ya eneo lake la ardhi. Hata hivyo, kufikia mwaka 2024, wilaya hiyo imepoteza hekta 14,000 za misitu (sawa na hekari 35,000).
Uharibifu huu umesababisha uzalishaji wa tani milioni 5.4 za hewa ya ukaa (carbon dioxide), hali inayochochea mabadiliko mabaya ya tabianchi na magonjwa ya mifumo ya upumuaji.
Sheria ya Misitu Namba 14 ya mwaka 2002, katika kifungu cha 49, inakataza shughuli zote za uvunaji wa mazao ya misitu bila kibali. Licha ya uwepo wa sheria hii na jitihada za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), uharibifu unaendelea katika maeneo mengi.
Kilimo Kinaangamia: Ushuhuda wa Wakulima
Mabadiliko ya tabianchi yameathiri vibaya sekta ya kilimo, ambayo ndiyo muhimili mkuu wa uchumi wa Chunya, ikiajiri takriban asilimia 87 ya wakazi wake. Wakulima wengi wanaripoti kushuka kwa kasi kwa uzalishaji wa mazao kutokana na mvua zisizotabirika.
Bi. Juliana Jeremiah, mkulima kutoka Kata ya Sangambi, anasimulia kwa masikitiko jinsi maisha yake yalivyobadilika:
“Mimi nimekuwa mmoja kati ya wakulima wazuri wa mahindi na maharage kwa miaka mingi… Nilikuwa nikipata mafanikio, watoto wanasoma na familia inaenda vyema. Lakini miaka hii ya karibuni imekuwa tofauti. Mvua zimekuwa chache sana na uhaba wa mvua umekuwa mkubwa. Ukataji wa miti na uchomaji mkaa unatubomoa.”
Bi. Juliana anaongeza kuwa hapo awali alikuwa akivuna kati ya magunia 15 hadi 20 ya mahindi kwa hekari, lakini sasa anavuna magunia matatu hadi tano pekee. Hali hii imemlazimu kuacha kilimo na kukimbilia biashara ya kuendesha mgahawa ili kujikimu, ingawa changamoto bado ni nyingi.
Mzee Charles Mweigomole (79) anakumbuka jinsi Chunya ilivyokuwa katika miaka ya 1980 hadi 1990:
“Kipindi hicho tulikuwa na misitu minene na mvua za kutosha. Mvua ikiamua kunyesha mwezi wa kumi, ilikuwa inanyesha kweli hadi mwezi wa nne. Lakini sasa hivi, mvua inanyesha mwezi wa nane kidogo, inakata, inakuja mwezi wa tisa au wa kumi kidogo… Huu uharibifu wa mazingira ndio unaoharibu mifumo ya mvua.”
Mtazamo wa Kitaalamu wa Kilimo
Raymond Choga, Afisa Kilimo wa Kata ya Sangambi, anathibitisha kuwepo kwa ongezeko la joto na mvua zisizotabirika ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Ili kukabiliana na hali hii, anashauri:
Mgogoro wa Maji na Changamoto za Kijamii
Ukataji wa miti umekausha vyanzo muhimu vya maji vilivyokuwa vikitiririka mwaka mzima, vikiwemo mito ya Mkola na Makongorosi. Kukauka kwa vyanzo hivi kumetengeneza changamoto kubwa ya kijamii, hususan kwa wanawake na watoto.
Bi. Rehema Adamson, mkazi wa Kijiji cha Sangambi, anaeleza adha wanayoipata:
“Tunapitia changamoto kubwa ya maji, hasa kipindi hiki cha kiangazi vyanzo vingi vimekauka. Tunalazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji. Hali hii inasababisha watoto kuchelewa au kushindwa kwenda shule kwa wakati.”
Adha hii haijaishia hapo; Bi. Rehema anabainisha kuwa uhaba huu wa maji umekuwa chanzo cha migogoro ya kifamilia. Wanawake wanapochelewa kurudi majumbani kwa sababu ya kutafuta maji umbali mrefu, waume zao wanakuwa hawaelewi, jambo linalozalisha ugomvi wa kifamilia.
Takwimu za Hali ya Hewa na Athari za Kiafya
Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bwana Eli Lipiki, anathibitisha kisayansi uwepo wa mabadiliko hayo.
Ndani ya kipindi cha miaka mitano (2021–2025), halijoto katika Wilaya ya Chunya imeongezeka kwa kati ya nyuzi joto (Degrees Centigrade).
Wakati huohuo, kiwango cha mvua kimeshuka kwa kasi kutoka milimita 1,500 kwa mwaka 2000 hadi kufikia milimita 800 pekee kwa mwaka 2025.
Athari kwa Sekta ya Afya
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Daktari Zuberi Mzige, anaeleza kuwa uharibifu wa misitu una athari za moja kwa moja kwa afya ya binadamu. Misitu inapopotea, kiwango cha hewa safi ya oksijeni (oxygen) kinashuka huku hewa ukaa (carbon dioxide) ikiongezeka.
Dkt. Mzige anataja athari kuu za kiafya zinazojitokeza Chunya kwa sasa kuwa ni pamoja na:
Wito wa Hatua na Suluhisho
Ili kunusuru Wilaya ya Chunya isigeuke kuwa jangwa kamili, Dkt. Mzige na wataalamu wengine wanatoa wito kwa Serikali na wadau wa mazingira kuongeza mikakati thabiti ya utoaji elimu endelevu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kupanda miti.
Aidha, kuna haja kubwa ya kuhamasisha na kuwezesha matumizi ya teknolojia mbadala za nishati kama vile mkaa mbadala unaotengenezwa kwa makaratasi na takataka ili kupunguza utegemezi mkubwa wa mkaa wa miti asili. Bila hatua za makusudi, mustakabali wa mazingira, uchumi, na afya ya wana-Chunya upo hatarini.
Andiko la: Mwanaisha Makumbuli
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.