Highlands FM

EU yalaumiwa kukwamisha fedha za tabianchi

18 November 2026, 3:05 pm

Mkurugenzi wa Sera wa ActionAid Marekani, Brandon Wu

ActionAid imeilaumu Umoja wa Ulaya (EU) kwa kukwamisha majadiliano ya fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na mpito wa haki, huku nchi zilizoendelea zikiahidi dola milioni 50 pekee kwa Mfuko wa Kukabiliana na Tabianchi mwaka huu.

Na Mwanaisha Makumbuli

Umoja wa Ulaya (EU) umelaumiwa kwa kukwamisha majadiliano muhimu kuhusu fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na mpito wa haki, hatua inayotajwa kudhoofisha juhudi za kimataifa za kukabiliana na athari za tabianchi.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na Mtandao wa Climate Action Network pembezoni mwa mkutano wa COP unaofanyika nchini Uturuki, Mkurugenzi wa Sera wa ActionAid Marekani, Brandon Wu, amesema EU inaongoza katika kuzuia maendeleo ya majadiliano hayo.

Wu amesema nchi zilizoendelea zimeahidi kiasi cha dola milioni 50 pekee kwa Mfuko wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund) mwaka huu, huku zikikataa kujadili ongezeko mara tatu la fedha za kukabiliana na athari za tabianchi, licha ya makubaliano yaliyofikiwa mwaka jana mjini Belem, Brazil.

Amesema hali hiyo pia imejitokeza katika suala la mpito wa haki, ambapo nchi hizo hazitaki kuanzishwa kwa mfumo mpya wa kusaidia jamii na wafanyakazi katika mabadiliko kuelekea uchumi usiotegemea nishati ya kisukuku, licha ya makubaliano yaliyofikiwa awali.

Wu amesema nchi zilizoendelea zimekuwa na tabia ya kukubaliana maamuzi katika mikutano ya kimataifa, lakini baadaye kuyadhoofisha katika mikutano inayofuata, akitolea mfano makubaliano ya mpito wa haki yaliyofikiwa Belem na Mfuko wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu ulioanzishwa mjini Sharm El Sheikh.

Ameonya kuwa Umoja wa Ulaya unakwamisha fursa ya kuimarisha mpito wa haki, badala ya kuunga mkono hatua zinazolenga kulinda jamii zilizoathirika na mabadiliko ya tabianchi.

Wu ameitaka EU kuacha kuzuia majadiliano na kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa, akisisitiza kuwa nchi zilizoendelea zinapaswa kuwajibika katika kutoa fedha na kuhakikisha haki kwa nchi zinazoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi.