Highlands FM

Wafanyabiashara Mbeya walalamikia bidhaa bandia

11 October 2026, 10:36 am

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, (SACP) Benjamin Kuzaga akiongea na Wafanyabiashara; Picha na Samwel Mpogole

Bidhaa bandia, gharama za usafirishaji na ushindani wa kibiashara! wafanyabiashara wa Mbeya wafunguka kuhusu changamoto zinazohatarisha mitaji yao. Je, Serikali itachukua hatua gani?

Na Samwel Mpogole

Wafanyabiashara wa Soko la SIDO na Mwanjelwa jijini Mbeya wameiomba Serikali kudhibiti bidhaa bandia zinazoingia sokoni, wakieleza kuwa zinawaingizia hasara na kuhatarisha mitaji yao, huku wakitaja pia gharama za usafirishaji na ushindani wa kibiashara kuwa miongoni mwa changamoto zinazowakabili.

Wakizungumza wakati wa kampeni ya Ongea na Kamanda, wafanyabiashara hao wameeleza kuwa baadhi yao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya bidhaa bandia ambazo, kwa mujibu wao, ni vigumu kuzitambua zinapotoka, licha ya kuathiri biashara zao na kuwaweka katika hatari ya kupata hasara, hasa wale wanaotegemea mikopo kuendesha shughuli zao.

Aidha, wamelalamikia baadhi ya daradara zinazokatisha safari hali wanayodai kuongeza gharama za usafirishaji, pamoja na matangazo ya biashara yanayofanywa kwa kutumia magari na sauti kubwa, ambayo wanadai wakati mwingine huleta usumbufu na kushusha thamani ya biashara za wenzao.

Sauti za Wafanyabiashara

Akizungumza katika kampeni hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga, amewataka wafanyabiashara hao kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu na watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu, akisisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kuimarisha usalama wa watu na mali zao.

Sauti ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya SACP Benjamin Kuzaga

Kampeni ya Ongea na Kamanda inalenga kuwapa wananchi fursa ya kuwasilisha maoni na changamoto zao za kiusalama moja kwa moja kwa Jeshi la Polisi, ili kuimarisha ushirikiano kati ya jeshi hilo na jamii.

Baadhi ya wafanyabiashara wakiongea mbele ya kamada Kuzaga