Highlands FM
Highlands FM
19 November 2026, 4:36 pm

Wanaharakati wa masuala ya tabianchi wamezitaka nchi tajiri kutekeleza ahadi ya kuanzisha mfumo wa Mpito wa Haki (Just Transition Mechanism), wakizituhumu kurejea nyuma katika makubaliano ya Belém, Brazil. Wamesema nchi zinazoendelea zinahitaji fedha na msaada wa kutosha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhamia nishati safi bila kuongezewa mzigo wa madeni.
Na Mwanaisha Makumbuli
Wanaharakati wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi wamezitaka nchi tajiri kutekeleza ahadi ya kuanzisha mfumo wa Mpito wa Haki (Just Transition Mechanism), wakizituhumu kurejea nyuma katika makubaliano yaliyofikiwa mwaka jana mjini Belém, Brazil.
Wakizungumza katika tukio la maandamano ya picha yaliyofanyika pembezoni mwa mkutano wa COP31 mjini Antalya, Uturuki, wanaharakati hao wamesema nchi zinazoendelea hazipaswi kuachwa kubeba mzigo wa mabadiliko ya tabianchi bila fedha, mipango na msaada wa kutosha.
Mwanaharakati wa masuala ya tabianchi kutoka Zambia, Valepi Banda, amesema jukumu la mpito wa nishati safi linaendelea kuelekezwa kwa nchi ambazo hazikuchangia kwa kiwango kikubwa uchafuzi wa mazingira.
Amesema hali hiyo inazikosesha nchi hizo uwezo wa kufanya mabadiliko ya kiuchumi na kukabiliana na athari za tabianchi.

Kwa upande wake, Junior Aleixo, Mratibu wa Sera na Programu wa ActionAid Brazil, amesema nchi tajiri zinapaswa kutimiza wajibu wao wa kihistoria kwa kusaidia nchi zinazoendelea, badala ya kuziongezea mzigo wa madeni katika kufadhili mpito wa nishati.
Wanaharakati hao wameitaka COP31 kuhakikisha ahadi ya kuanzisha mfumo wa Mpito wa Haki inatekelezwa, ili kulinda jamii zilizoathirika na mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha mabadiliko kuelekea nishati safi yanafanyika kwa haki.