Highlands FM
Highlands FM
5 October 2026, 4:13 pm

Darasa janja limeanza kubadili namna wanafunzi wa kike Garijembe wanavyojifunza sayansi!Je, TEHAMA imewapa hamasa gani? kwa nini darasa hili limekuwa kivutio kwa wanafunzi
Na Samwel Mpogole
Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imeendelea kutumia TEHAMA kuboresha mazingira ya kujifunzia, hatua ambayo imeanza kuongeza hamasa kwa wanafunzi wa kike katika Shule ya Sekondari Garijembe kujifunza masomo ya sayansi.
Wanafunzi hao sasa wanatumia darasa janja lenye mfumo wa kidijitali unaowawezesha kupata vitabu, picha na maudhui mbalimbali ya masomo kupitia kompyuta, hali inayowarahisishia kuelewa mada na kujifunza kwa njia shirikishi zaidi.
Matumizi ya teknolojia hiyo pia yameanza kubadili namna walimu wanavyowasilisha masomo, kwa kutumia picha, mifano na maudhui ya kidijitali yanayowafanya wanafunzi kuyaona na kuyaelewa kwa urahisi.
Mbali na kurahisisha ufundishaji, mfumo huo unawawezesha wanafunzi kupata vitabu vyao kidijitali, huku kila mwanafunzi akiwa na akaunti yake ya kuingia na kujifunza.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwa kuwekeza katika TEHAMA, akieleza kuwa matumizi ya teknolojia katika shule za wasichana yanaweza kuwa kichocheo muhimu cha kuongeza ushiriki wao katika masomo ya sayansi.
Hatua hiyo inaendelea kuonyesha namna TEHAMA inavyoweza kubadili mazingira ya kujifunzia na kuwapa wanafunzi, hususan wasichana, fursa ya kujifunza sayansi kwa njia ya kisasa na yenye kuwavutia zaidi.
