Highlands FM
Highlands FM
28 May 2026, 11:39 am

(TBS) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini imewataka wanaume kuwa karibu na wenza wao katika kufuatilia matumizi ya vipodozi ili kuhakikisha bidhaa zinazotumika ni salama kwa afya na zinakidhi viwango vinavyokubalika.
Na Samwel Ndoni,
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini limewataka wanaume kuwa karibu na wenza wao katika kufuatilia matumizi ya vipodozi wanavyotumia, kwa kuhakikisha bidhaa hizo zinakuwa salama kwa afya na zenye viwango vinavyokubalika.
Wito huo umetolewa jana jijini Mbeya na Kaimu Meneja wa TBS Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Rodney Alananga, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya biashara na uwekezaji ya Mbeya City Expo.
Alananga alisema kuwa ongezeko la matumizi ya vipodozi vyenye kemikali hatari limeendelea kuwa tishio kwa afya ya wananchi, huku baadhi ya watumiaji wakikumbwa na madhara makubwa ya ngozi kutokana na matumizi ya bidhaa zisizo salama.
Alisema ni muhimu kwa jamii kuacha kuchukulia suala la vipodozi kama jambo la wanawake pekee, kwani hata wanaume wamekuwa waathirika wa matumizi ya bidhaa zenye viambata vyenye sumu.
“Leo hii hata baadhi ya vipodozi vinavyotumiwa na wanaume vina madhara kiafya. Mfano ni mafuta aina ya Clair Men ambayo uchunguzi umeonyesha yanaweza kusababisha madhara ya muda mfupi na muda mrefu, ikiwemo saratani ya ngozi,” alisema Alananga.
Aidha, aliwataka wananchi kuwa makini wanaponunua vipodozi kwa kuhakikisha bidhaa hizo zina nembo ya ubora kutoka TBS pamoja na taarifa sahihi za mtengenezaji.
Alisema matumizi ya vipodozi visivyo salama yanaweza kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo kubabuka kwa ngozi, mabadiliko ya rangi ya ngozi, mzio, uharibifu wa ngozi na hata magonjwa sugu yanayoweza kuhatarisha maisha.
Kwa mujibu wa Alananga, TBS imeendelea kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya vipodozi vyenye viambata hatarishi ili kuwasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi wanaponunua bidhaa hizo.
Hata hivyo, alisema taasisi hiyo haiwezi kufanikisha mapambano dhidi ya bidhaa hatarishi bila ushirikiano wa wananchi, wafanyabiashara na wadau wengine wa afya.
“Tunawahimiza wananchi kutoa taarifa wanapobaini bidhaa zinazotiliwa shaka ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.
Ushirikiano wa jamii ni muhimu sana katika kuhakikisha bidhaa zisizo salama zinaondolewa sokoni,” alisema.
Aliongeza kuwa TBS imekuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka, masoko na vituo vya biashara ili kubaini bidhaa zisizokidhi viwango pamoja na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wanaokiuka sheria.
Mbali na ukaguzi, Alananga alisema TBS imekuwa ikitumia majukwaa mbalimbali ya elimu kwa umma ikiwemo maonesho ya biashara, mikutano ya wazi na vipindi vya redio na televisheni ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Alisema maonesho ya Mbeya City Expo yamekuwa jukwaa muhimu kwa taasisi hiyo kukutana na wananchi ana kwa ana na kutoa elimu kuhusu matumizi salama ya bidhaa mbalimbali zinazotumiwa katika maisha ya kila siku.
Baadhi ya wananchi waliofika kwenye banda la TBS katika maonesho hayo walieleza kufurahishwa na elimu inayotolewa, wakisema imewasaidia kuelewa namna ya kutambua bidhaa salama na kuepuka bidhaa zenye madhara.
Mmoja wa wananchi hao, Juliana Frank alisema watu wengi wamekuwa wakinunua vipodozi kwa kuangalia matokeo ya haraka bila kujali madhara yanayoweza kujitokeza baadaye.
“Nimejifunza kuwa si kila bidhaa inayouzwa sokoni ni salama. Kuna umuhimu mkubwa wa kusoma maelekezo ya matumizi na kuhakikisha bidhaa imethibitishwa na TBS kabla ya kuitumia,” alisema.
Wafanyabiashara wa vipodozi nao wametakiwa kuhakikisha wanauza bidhaa zilizosajiliwa na kuthibitishwa ili kulinda afya za wateja wao pamoja na kuepuka hatua za kisheria.
Alananga alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya bidhaa bandia na zisizo salama yanahitaji ushirikiano wa kila mmoja, huku akiwataka wananchi kuendelea kuwa mabalozi wa matumizi salama ya bidhaa katika jamii.
Alisema TBS itaendelea kuimarisha udhibiti wa bidhaa nchini kwa lengo la kuhakikisha afya na usalama wa watumiaji vinapewa kipaumbele wakati wote.