Highlands FM
Highlands FM
9 June 2026, 3:10 pm

Na Samwel Mpogole Mussa
Kutoka mashamba ya Kyela hadi masoko ya dunia, Farm to Table Tourism inabadilisha kilimo kuwa utalii na ajira. Cocoa, kahawa na parachichi sasa si mazao tu bali ni daraja jipya la uchumi unaounganisha wakulima, wawekezaji na watalii. Safari inaanzia shambani… na kuishia mezani.
Katika kijiji cha Mababu wilayani Kyela, mkoani Mbeya, sauti ya mashamba ya Cocoa, harufu ya nzuri ya Cocoa iliyokaushwa na mandhari ya mashamba ya parachichi vinaunda picha mpya ya Tanzania ya leo.
Hapa, kilimo hakibaki kuwa na sura hiyo pekee.Kinakuwa utalii.Kinakuwa biashara.Na kinakuwa chanzo cha hadithi mpya ya uchumi.
Ndani ya mabadiliko haya, anasimama Kristopha Mwasambili, mzee mwenye umri wa miaka 70, Mkurugenzi wa LIVY Africa Ltd, ambaye ameweka jina la Kyela kwenye ramani ya bidhaa za cocoa zilizoongezwa thamani.
Lakini safari yake si ya peke yake.Ni sehemu ya mabadiliko makubwa ya kitaifa. Kama wahenga wasemavyo “ukitaka kwenda mbali nenda na wenzako na ukitaka kwenda haraka nenda pekeyako” kwa mzee Mwasambili akachagua kwenda mbali.
Kwa mujibu wa takwimu za Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na Benki Kuu ya Tanzania, Tanzania ilipokea watalii takribani milioni 5.36 mwaka 2024, idadi ambayo iliongezeka hadi karibu milioni 5.94 mwaka 2025.
Mapato ya sekta hiyo yakafikia zaidi ya dola bilioni 4.4 kwa mwaka, huku utalii ukichangia takribani asilimia 17 ya Pato la Taifa.
Lakini sasa, aina mpya ya utalii inaongezeka haraka utalii wa kilimo na chakula, maarufu kama Farm to Table Tourism.
Utalii unaomruhusu mgeni kuona chakula na bidhaa kuanzia shambani hadi mezani.Ndani ya Kyela, cocoa imekuwa zaidi ya zao la biashara.Kwa mujibu wa takwimu za Wilaya, zaidi ya tani 9,000 za cocoa zinazalishwa katika baadhi ya misimu hususani msimu uliopita.
Lakini tofauti kubwa sasa ni moja: thamani inaongezwa ndani ya nchi.Hapa ndipo LIVY Africa Ltd inapoingia.
Kristopha Mwasambili anasema kwa miaka mingi Tanzania imekuwa ikipoteza faida kubwa kwa kuuza malighafi bila kuongezwa thamani.
“Leo tunaona mabadiliko makubwa. Cocoa inayolimwa Kyela sasa inabadilishwa kuwa chocolate na bidhaa nyingine zinazoweza kushindana sokoni ndani na nje ya nchi,” anasema.
Mabadiliko haya yamewezeshwa pia na mazingira bora ya uwekezaji na sera za serikali zinazohamasisha viwanda na kuongeza thamani ya mazao.
Mwasambili anasema sasa Tanzania imeanza kuvutia wawekezaji na kurahisisha mnyororo wa uzalishaji.
“Leo tunaona mazingira yanazidi kuwa bora. Wawekezaji wanaweza kufanya kazi kwa urahisi zaidi, na wakulima wananufaika moja kwa moja na soko la bidhaa zao,” anasema.
Katika maeneo ya Kyela na Mbeya, watalii sasa hawaji kuangalia wanyamapori pekee.Wanakuja kuona:Kahawa inavyolimwa, Cocoa inavyosindikwa na Parachichi linavyovunwa
Huu ni utalii unaounganisha kilimo na chakula, ukibadilisha mashamba kuwa vivutio vya utalii.

Katibu wa AMCOS ya Mababu, Jeremia Anderson, anasema wakulima sasa wanafaidika zaidi kupitia uongezaji wa thamani na soko la moja kwa moja.
“Kabla tulikuwa tunategemea wanunuzi wa kati, lakini sasa wageni wanakuja mashambani na kununua moja kwa moja, jambo linaloongeza kipato cha mkulima,” anasema.
Mkurugenzi wa Operesheni na Udhibiti Ubora kutoka COPRA, Kamwesige Mtembei, anasema ubora wa bidhaa ndio msingi wa ushindani wa kimataifa.
“Tanzania inaweza kushindana duniani endapo tu tutaweka mkazo kwenye ubora wa bidhaa zetu,” anasema.
Mtafiti wa TARI, Daudi Mbongo, anasema utafiti umeongeza uzalishaji na ubora wa mazao kama cocoa, kahawa na parachichi kupitia mbegu bora na teknolojia.
“Kazi yetu ni kuhakikisha mkulima anapata teknolojia sahihi inayoongeza tija na ubora,” anasema.
Parachichi limekuwa miongoni mwa mazao yanayokua kwa kasi nchini Tanzania.Kwa mujibu wa takwimu za sekta ya kilimo, Tanzania huzalisha zaidi ya tani 200,000 kwa mwaka, huku kati ya tani 30,000 hadi 40,000 zikiuzwa nje ya nchi.
Ukuaji wa mauzo ya nje umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 60 hadi 70 katika miaka ya hivi karibuni.Mkulima kutoka Kiwira Obadia Mwangoka anasema sasa parachichi limekuwa chanzo kikubwa cha kipato.
“Leo mkulima anaona thamani ya kazi yake tofauti na zamani. Soko la nje limeongeza matumaini mapya,” anasema.
Farm to Table Tourism haijanufaisha wakulima pekee. Imefungua ajira kwa vijana kama waongozaji wa watalii, watengenezaji wa maudhui, wafanyabiashara wa chakula na huduma za usafiri.
Kama ilivyo dunia ya sasa Teknolojia imekuwa na mchango mkubwa katika Nyanja mbali mbali na hapa MC Mboneke anathibitisha namna mitandao ya kijamii imekuwa na mchango mkubwa kuitangaza Kyela na Mbeya kwaujumla.
“Wageni wengi wanakuja baada ya kuona video za mashamba na chakula mtandaoni,” anasema.
Mama Anna mjasiliamari mwenye watoto wawili kutoka kijiji cha mababu, anasema wanawake sasa wanapata soko kupitia huduma za chakula na bidhaa za asili.
“Watalii wanapokuja, tunapata fursa ya kuuza na kutoa huduma, jambo linaloongeza kipato cha familia zetu na hata kwenye mikutano na mikusanyiko mbali mbali utakutana na kinama tukiuza bidhaa,” anasema.
Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Josephine Manase, anasema cocoa na mazao mengine sasa ni zaidi ya kilimo ni fursa ya utalii na uwekezaji.
“Cocoa ya Kyela ni mfano wa jinsi kilimo kinavyoweza kuunganishwa na utalii na biashara,” anasema.
Kutoka mashamba ya kahawa, cocoa na parachichi hadi viwanda vya kuongeza thamani na meza za watalii, Tanzania inaandika simulizi mpya.Simulizi ya uchumi unaotokana na ardhi.Simulizi ya ajira zinazozalishwa na kilimo.Na simulizi ya utalii unaoanzia shambani na kuishia mezani.
Na katikati ya safari hiyo, kuna mzee Kristopha Mwasambili na wadau wengine waliobadilisha wazo kuwa uhalisia na Kyela kuwa sehemu ya ramani ya uchumi mpya wa Tanzania.

