Highlands FM

Hedhi si hofu tena: jinsi elimu na huduma maalum zinavyobadili maisha ya wasichana wenye ulemavu Mbeya

9 June 2026, 11:56 am

Picha ni Mama Nelly akitoa Elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu juu ya matumizi ya taulo za kike.

Makala hii inaangazia namna elimu ya hedhi salama, huduma za afya na vituo vya ESRAC vinavyowasaidia wasichana wenye ulemavu kujitambua, kujiamini na kuendelea na masomo bila kuachwa nyuma.

Na Samwel Mpogole Mussa.

Damu ilipoanza kutoka kwa mara ya kwanza, hakuelewa kilichokuwa kinaendelea.Aliogopa.Akalia.Akadhani amejeruhiwa.Hakuna aliyekuwa amemwandaa kuelewa maana ya hedhi.

Kwa sababu ya hali yake ya ulemavu wa akili, ilikuwa vigumu kwake kufahamu kwa haraka mabadiliko yaliyokuwa yanatokea ndani ya mwili wake.

Hii ndiyo hali inayowakabili baadhi ya watoto wa kike wenye ulemavu nchini Tanzania wanapoingia balehe.

Lakini leo, simulizi hiyo inaanza kubadilika.Katika nyumba moja jijini Mbeya, Mama Nelly amejitolea maisha yake kuwahudumia zaidi ya watoto 70 wenye ulemavu waliotelekezwa, waliotupwa au waliotoka katika mazingira magumu wakiwa na ulemavu.

Mbali na kuwapatia makazi na malezi, amekuwa mstari wa mbele kuwasaidia watoto hao kuelewa mabadiliko ya miili yao, hususan kipindi cha hedhi.

“Wengine hawaelewi kabisa maana ya hedhi. Wanapoona damu wanaogopa. Lakini tukiwafundisha hatua kwa hatua, wanaanza kuelewa na kujiamini,” anasema.

Kwa Mama Nelly, hedhi si suala la afya pekee, bali ni suala la heshima na haki za mtoto.

Kwa mujibu wa UNICEF, zaidi ya wanawake na wasichana bilioni 1.8 duniani hupata hedhi kila mwezi huku watoto milioni 240 duniani wakiishi na aina mbalimbali za ulemavu.

Takwimu hizo zinaonyesha umuhimu wa kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata elimu sahihi ya afya ya uzazi na hedhi salama.

Nchini Tanzania, juhudi mbalimbali zimeendelea kufanyika kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma.

Daktari Joy kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mbeya anasema watoto wenye ulemavu wanahitaji maandalizi maalumu ili kuwawezesha kuelewa mabadiliko wanayopitia.

“Mtoto mwenye ulemavu anahitaji kufundishwa kwa lugha rahisi na kwa hatua zinazomfaa. Akielewa kinachoendelea, hofu hupungua na anajenga uwezo wa kujitunza,” anasema.

Mbali na sekta ya afya, wadau wa maendeleo nao wameendelea kusaidia juhudi za kuwafikia watoto hawa.

Mkurugenzi wa Kampeni ya Binti Tanzania Ngara, Wamuzi Hasan, anasema kwa zaidi ya miaka mitano kampeni hiyo imeendelea kuwafikia mamia ya mabinti kwa kuwapatia elimu ya afya ya uzazi, vifaa vya hedhi na msaada wa kisaikolojia.

“Tumeona mabinti wengi wakiongeza kujiamini baada ya kupata elimu sahihi. Elimu ndiyo silaha kubwa ya kuondoa hofu na unyanyapaa,” anasema.

Wakati huo huo, Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuimarisha mfumo wa elimu jumuishi kupitia uanzishaji wa Vituo vya Upimaji, Utambuzi na Rasilimali za Elimu kwa Watoto (ESRAC).

Vituo hivyo vinalenga kutambua mapema changamoto za watoto na kuwaunganisha na huduma stahiki za elimu na maendeleo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha matumizi ya vituo vya ESRAC jijini Mbeya, Mkuu wa Mkoa wa mbeya Beno Malisa alisema vituo hivyo ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha kila mtoto anapata fursa sawa ya elimu.

Mpaka sasa Halmashauri 36 zinatekeleza mpango wa ESRAC huku utekelezaji wa agizo hilo ukiendelea kuongezeka hatua kwa hatua, jambo linalowezesha watoto wengi zaidi kufikiwa na huduma za utambuzi wa mapema.

Mkurugenzi wa HakiElimu, Marry Ndaro, anasema huduma hizo zimeanza kuleta matokeo chanya kwa watoto wengi wenye mahitaji maalumu.

“Kadiri vituo vinavyoongezeka, ndivyo watoto wengi zaidi wanavyopata nafasi ya kutambuliwa mapema na kupata msaada wanaouhitaji,” anasema.

Katika Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya, ambako kuna kituo cha ESRAC, Mkuu wa kituo hicho Mwalimu Aida Mwakalukwa anasema uelewa wa wazazi umeanza kuongezeka ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

“Kuna wazazi wengi zaidi sasa wanaofika kutafuta ushauri na huduma za utambuzi kwa watoto wao. Hii ni hatua kubwa,” anasema.

Picha Siku ya uzinduzi wa kituo cha ESRAC Jamii ikipewa elimu shule ya mwenge Mbeya.

Kwa upande wake, Angela Chales ambaye ni mzazi wa mtoto mwenye uhitaji maalumu, anasema huduma hizo zimemsaidia kuelewa namna bora ya kumlea mwanawe.

“Nilipata ushauri na nikaanza kuona mabadiliko. Leo najua mtoto wangu hahitaji lawama, anahitaji msaada na kueleweka,” anasema.

Kwa watoto wa kike wenye ulemavu, huduma hizi zina maana kubwa zaidi.Zinawasaidia kuelewa miili yao.Zinawasaidia kujiamini.Na zinawapa nafasi ya kuendelea na masomo bila kuachwa nyuma.

Leo, ndani ya nyumba ya Mama Nelly, baadhi ya wasichana ambao waliwahi kuogopa hedhi wanaanza kuielewa na kuikubali kama sehemu ya maisha yao.

Kupitia juhudi za wazazi, walezi, wataalamu wa afya, wadau wa maendeleo na Serikali, matumaini yanaendelea kurejea kwa watoto wengi wenye mahitaji maalumu.

Lakini kwa kila mtoto anayepata elimu kuhusu hedhi salama, kwa kila mzazi anayepata uelewa, na kwa kila kituo cha ESRAC kinachoanzishwa, Tanzania inapiga hatua moja zaidi kuelekea jamii inayomwona kila mtoto kuwa na thamani sawa.

Kwa sababu hedhi si aibu.Ulemavu si kikwazo cha ndoto.Na kila mtoto anastahili nafasi ya kuishi, kujifunza na kufanikiwa.

Mwanafunzi mwenye mahitaji maalumu akijumuika nawenzake kuelekea shule kutokana na mazingira rafiki ya uwepo kituo cha ESRAC