Highlands FM
Highlands FM
13 October 2026, 10:40 am

Watu wenye ulemavu watajwa miongoni mwa wanufaika wenye changamoto ya kurejesha mikopo ya asilimia 10 Chunya, huku madeni ya vikundi katika baadhi ya kata yakifikia shilingi milioni 600.
Na Samwel Mpogole
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Tamim Kambona, ameonya kuwa wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 watakaoshindwa kurejesha fedha hizo kwa muda uliopangwa watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kufikishwa mahakamani.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kambona amesema halmashauri hiyo imetoa zaidi ya shilingi bilioni moja kwa vikundi vya wanufaika, lakini kasi ya urejeshaji wa mikopo hiyo bado hairidhishi, hali inayoweza kuathiri upatikanaji wa fedha hizo kwa vikundi vingine vinavyostahili kunufaika.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Chunya, Esther Kondobole, amesema baadhi ya kata zina vikundi vyenye madeni ya jumla ya takribani shilingi milioni 600, huku akieleza hatua zinazochukuliwa kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa.
Kondobole ameongeza kuwa vikundi vya vijana na watu wenye ulemavu ni miongoni mwa vinavyoongoza kwa kuwa na mikopo chechefu, hali inayozua changamoto katika usimamizi na urejeshaji wa fedha hizo.
