Highlands FM

ActionAid International yazitaka serikali kukataa rasimu ya maamuzi ya COP31

22 November 2026, 2:51 pm

Mkuu wa Masuala ya Haki ya Tabianchi wa shirika hilo, Teresa Anderson {Picha kutoka kwa ActionAid}

ActionAid International imezitaka serikali kukataa rasimu ya maamuzi ya COP31, ikisema imeshindwa kuweka fedha za kusaidia jamii zinazokabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Na Mwanaisha Makumbuli

Shirika la kimataifa la ActionAid International, lenye makao makuu Johannesburg, Afrika Kusini, limezitaka serikali kukataa rasimu ya maamuzi ya mwisho ya mkutano wa COP31, likisema imeshindwa kuweka mikakati madhubuti ya kifedha kusaidia jamii zinazokabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mkuu wa Masuala ya Haki ya Tabianchi wa shirika hilo, Teresa Anderson, amesema rasimu hiyo inarudisha nyuma juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kutokana na kudorora kwa ahadi za fedha na kupewa nafasi kwa suluhisho zinazodaiwa kutokuwa sahihi.

Amesema hali hiyo inawaweka katika hatari zaidi wananchi walio mstari wa mbele kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ambao wanahitaji msaada wa kifedha na hatua madhubuti za kukabiliana na changamoto hizo.

Aidha, Anderson ameonya kuwa rasimu hiyo inaonekana kutoa nafasi kwa makampuni ya mafuta ya kisukuku na teknolojia kubwa kunufaika kupitia miradi ya kukamata hewa ukaa, badala ya kuzingatia mahitaji ya jamii zilizoathirika.

Amesisitiza kuwa serikali zinapaswa kuweka mbele maslahi ya wananchi kwa kuhakikisha kunakuwa na fedha za kutosha na mikakati inayotekelezeka ili kusaidia jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.