Highlands FM
Highlands FM
5 November 2026, 2:50 pm

TAKUKURU Mbeya yarejesha fedha za wananchi waliotapeliwa kwa ahadi za nafasi za kujiunga na JKT, huku ikiokoa pia milioni 4.5 zilizotokana na uuzaji wa eneo la kijiji
Na Samwel Mpogole
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mbeya imewatahadharisha wananchi kutokubali kurubuniwa na baadhi ya watu wanaodai kuwa na uwezo wakuwaunganisha na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kwakuwataka watoe fedha, kwani nafasi hizo hutolewa bure
Tahadhari hiyo inatolewa baada ya TAKUKURU kubaini vitendo vya rushwa vilivyowahusisha wananchi wawili waliotoa jumla ya shilingi 350,000 kwa mtu aliyewaahidi kuwasaidia kupata nafasi za kujiunga na JKT Wilaya ya Rungwe.
Akizungumza na waandishi wa habari, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya, Jasper Luoga, amesema taasisi hiyo imefanikiwa kurejesha fedha hizo kwa walalamikaji katika kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026.
Luoga amewataka wananchi kutumia njia rasmi wanapotafuta fursa za ajira na kujiunga na taasisi mbalimbali ili kuepuka kuingia katika mikono ya watu wanaotumia mianya hiyo kujipatia fedha kwa njia zisizo halali.
Katika hatua nyingine, TAKUKURU Mkoa wa Mbeya imefanikiwa kurejesha shilingi milioni 4.5 katika akaunti ya Kijiji cha Mwampalala kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, baada ya kubaini kuwa viongozi wa kijiji hicho waliuza eneo la kijiji na kutumia fedha zilizopatikana kwa matumizi binafsi.
