Highlands FM

Madereva 8 Wafungiwa Leseni Mbeya

4 October 2026, 8:19 pm

Picha ya magari yakiwa katika barabara kuu Tanzam; Picha na Samwel Mpogole

Zikiwa zimepita siku chache tangu mgomo wa madereva wa mabasi, Jeshi la Polisi Mbeya limetoa taarifa kuhusu usalama barabarani na kuwafungia leseni madereva 8 kwa makosa hatarishi

Na Samwel Mpogole

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya katika kipindi cha mwezi watisa limewafungia leseni za udereva madereva nane kutokana na makosa hatarishi ya usalama barabarani, ikiwemo mwendo kasi na kuyapita magari katika maeneo yasiyoruhusiwa.

Akizungumzia hali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga, amesema hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya Jeshi hilo ya kuzuia ajali za barabarani na kuhakikisha madereva wanazingatia sheria na kanuni za usalama barabarani.

Aidha, Kuzaga amesema katika operesheni zilizofanyika mwezi Septemba, Jeshi hilo limewakamata Razaki Makolo na Luka Dotto, wakazi wa Mabatini, Chunya, kwa tuhuma za kumuua Sira John, mwenye umri wa miaka 20.

Amesema watuhumiwa hao wanadaiwa kumuua marehemu kwa kumchoma kwa kitu chenye ncha kali baada ya kutokea ugomvi wakati wakinywa pombe pamoja.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi hilo kwa kutoa taarifa za uhalifu na matukio yanayoweza kuhatarisha usalama katika jamii.