Karagwe FM

Wanaolima katika vyanzo vya maji Karagwe wapewa siku 7 kujisalimisha

9 October 2026, 11:43

Mkuu wa wilaya ya Karagwe Julius Laizer. Picha na Shabani Ngarama

Maeneo mengi ya wilaya ya Karagwe mkoani Kagera yameendelea kuripotiwa kuwa na changamoto ya upatikanaji maji toshelezi licha ya miradi kadhaa inayoripotiwa kutekelezwa hali inayoelezwa kuchangiwa na uwepo wa shughuli za kibinadamu katika vyanzo vichache vya maji vilivyopo

Na Shabani Ngarama, Karagwe

Mkuu wa wilaya ya Karagwe Julius Kalanga Laiser amewataka wananchi wanaofanya shughuli za kibinadamu hasa kilimo ndani ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji kuacha mara moja na kujisalimisha ndani ya siku 7.

Wananchi hao wanatakiwa kujiandikisha kwa kutaja majina yao na kuahidi kutorudia kufanya shughuli hizo, kabla ya ofisi yake kuanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watakaokaidi agizo hilo kwani shughuli hizo ni miongoni mwa sababu zinazochangia changamoto ya upungufu wa maji.

Laizer ametoa agizo hilo Oktoba 8, 2026 wakati wa ziara yake ya kikazi katika kijiji cha Nyakayanja, Kata ya Nyaishozi wakati akikagua miradi ya maendeleo ikiwemo Zahanati ya Nyaishozi, kusikiliza na kutatua kero za wananchi, pamoja na kutoa Tahadhari kuhusu maandalizi ya kukabiliana na mvua za El-Niño.

Sauti ya Mkuu wa wilaya ya Karagwe Julius Laizer
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Nyakayanja kata ya Nyaishozi wakishiriki mkutano. Picha na Shabani Ngarama
Diwani wa kata ya Nyaishozi Wallace Mashanda (wa kwanza kushoto) akiwa na mkuu wa wilaya ya Karagwe Julius Laize (mwenye kisemeo). Picha na Shabani Ngarama

Kwa upande wake, diwani wa kata ya Nyaishozi, Wallace Mashanda amesema, kata hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji na kuiomba serikali kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuunganisha njia za usambazaji maji na kufanya uchaguzi upya wa kamati tendaji ya maji. Aidha, ameishukuru serikali kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata hiyo, ikiwemo shilingi milioni 50 kwa ajili ya ukarabati wa zahanati ya Nyaishozi na shilingi milioni 60 kwa ajili ya kukamilisha maabara za sayansi.

Sauti ya diwani wa kata ya Nyaishozi, Wallace Mashanda
Mkazi wa Nyakayanja akitoa kero zake kwa mkuu wilaya Julius Laizer. Picha na Shabani Ngarama