Karagwe FM

CBIDO yatoa milioni 20 kwa wenye ulemavu Karagwe

5 May 2024, 5:42 pm

Wa pili kushoto ni diwani wa kata Chanika Longino Wilbard akipokea taarifa ya watakao hudumiwa katika kata yake.Picha na Eliud Henry

Wako baadhi ya watoto wanaozaliwa wakiwa na ulemavu na wengine hupata ulemavu wanapokuwa wakubwa hivyo jamii haina budi kushirikiana kuwasaidia ili waweze kujikimu katika maisha.

Na Eliud Henry:

Kiasi cha Fedha sh. Mil 20 zimetolewa na shirika la kuwahudumia watu wenye ulemavu wilayani Karagwe CBIDO Kwa ajili huduma za utengamavu za moja kwa moja kwa walengwa waliopo katika kata za Chanika na Kamagambo wiliyani Karagwe.

Akizungumza May 3,2024 katika kikao maalumu kilichowakutanisha viongozi mbalimbali ngazi ya halmashauri ya wilaya,viongozi wa kata pamoja na watumishi wa shirika hilo Bwana Frolian Rwangoga ambaye ni mkurugenzi wa CBIDO amesema kuwa fedha hizo zilizotolewa ni kwa ajili ya huduma za utengamavu za moja kwa moja kwa watoto walioainishwa katika kitabu maalumu kilichoandaliwa kwa ajili ya kurahisisha mradi huo katika kata za Chanika na Kamagambo wilayani Karagwe.

Sauti ya Frolian Rwangoga ambaye ni mkurugenzi wa CBIDO

Bwana Rwangoga amesema kuwa watoto wote waliokuwa wakihudumiwa na CBIDO moja kwa moja sasa wataanza kuhudumiwa katika kata zao kwa kushirikiana na serikali ngazi ya halmashauri huku akieleza kuwa shirika hilo halitajihusisha na huduma za moja kwa moja kwa walengwa waliopo katika kata hizo badala yake wataendelea kuweka fedha kwenye account za kata na kamati maalumu zilizopo katika kata hizo ndizo zitashughulikia watoto hao moja kwa moja.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Karagwe Mhe.Wallace Mashanda amewataka viongozi wote kwenye kata husika kushirikiana ili kuhakikisha wanawahudumia walengwa ipasavyo jambo litakalochochea kupanua miradi mingine katika wilaya nzima na taifa kwa ujumla.

Sauti ya mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Karagwe Mhe.Wallace Mashanda

Naye mwezeshaji wa jamii katika kata ya Chanika Bi. Julieth Lewis amewataka viongozi na wahudumu katika kata hizo kuweka vizuri kumbukumbu za watu wenye ulemavu katika kata zao na kuhifadhi nyaraka zao mahali salama ili kutunza siri za watu wanao wahudumia.

Sauti ya mwezeshaji wa jamii katika kata ya Chanika Bi. Julieth Lewis

Ikumbukwe kuwa fedha zilizotolewa ni Milioni 20 ambapo milioni 10 zinaenda kuhudumu katika kata ya Chanika na nyingine zitahudumu katika kata ya Kamagambo na Shirika hilo linatarajia kuongeza fedha nyingine endapo fedha hizo zilizotolewa zitatumika ipasavyo.