Karagwe FM

Homa ya marburg Kagera yatokomezwa

2 June 2023, 10:17 pm

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ameutangazia ulimwengu kuwa Kagera na Tanzania ni salama dhidi ya ugonjwa wa marburg na kwamba hakuna tena ugonjwa huo. Pamoja na hayo waziri Ummy pia amewashukuru watumishi wa wizara ya afya pamoja na mashirika ya kimataifa kwa ushirikiano waliouonesha kwa kipindi chote cha mlipuko sambamba na kumshukru Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hatua iliyochukuliwa ya kutangaza uwepo wa ugonjwa huu na ndiyo maana mapambano yalifanyika kwa ushirikiano na hatimaye umemalizika.

Waziri Ummy amesema kuwa ugonjwa huu pamoja na kumalizika umechukua maisha ya watanzania 6 akiwemo daktari mmoja aliyehudumia waathirika kati ya watu 9 walioambukizwa. Amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwani hadi ugonjwa huo unamalizika haikujulikana wazi wapi ulipotokea zaidi ya kujua kuwa mlipuko ulionekana katika kata za Maruku na Kanyangereko wilayani Bukoba.