Karagwe FM

Jela miaka 30 kwa ubakaji wa mtoto

4 July 2023, 11:38 am

Mahakama ya wilaya ya Missenyi mkoani Kagera, imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela Mahmoud Idi (54) mkulima mkazi wa kijiji cha Kigarama kata ya Kanyigo wilayani humo kwa kuthibitika pasipo na shaka kuwa alimbaka mtoto wa miaka minane kijijini hapo (jina lake na shule anayosoma mtoto huyo vinahifadhiwa).

Hukumu hiyo imetolewa na hakimu wa mahakama hiyo ambaye pia ni hakimu mfawidhi wa wilaya, Yohana Myombo tarehe 15 Machi 2023.

Wakili wa serikali, Mkaguzi wa polisi  Zakayo Napegwa amesema Mahmoud Idi almaarufu Maalim, ametenda kosa hilo tarehe  26 Oktoba 2022 majira ya saa saba mchana baada ya kuletewa mzigo wa nyasi aliokuwa amemtuma mtoto huyo, kisha kumvuta chumbani kwa nguvu na kumbaka.

Baada ya kitendo hicho,mtoto alielekea nyumbani akilia na kumueleza mama yake ndipo taarifa zilitolewa kituo kidogo cha polisi Kanyigo ambapo mtuhumiwa alikamatwa.

Tarehe 21 Desemba 2022 mtuhumiwa alifikishwa mahakamani na hukumu kutolewa rarehe 15 Machi.

Baadhi ya wananchi  mkoani Kagera wameipongeza mahakama hiyo kwa kutenda haki,na kupigania maslahi ya watoto.

Abimeleck  Richard wa shirika lisilo la kiserikali la TADEPA mkoani Kagera,amesema ushirikiano wa kila mtu unahitajika katika kutoa taarifa za ukatili dhidi ya watoto ili kulinda haki zao.

Conchesta Kanywa,mwenyekiti wa kitongoji Rwagati, kijiji Bugombe, kata ya Kanyigo, ambaye pia ni mdau wa masuala ya watoto, ameshukuru kwa ushirikiano wa wadau kwa kulifikisha suala hili mahakamani,akisema kuna vitendo vya ukatili vinatokea lakini vinazimwa kwa nguvu ya fedha.