Karagwe FM

Askofu Bagonza: Acheni kuamini vitu vinavyoharibika

16 September 2023, 8:00 pm

Septemba 15, 2023 waumini wa kanisa la Kiinjili la kilutheri Tanzania Dayosisi ya Karagwe wamejumuika pamoja katika tamasha la nne la uimbaji la wanawake wa dayosisi hiyo ambapo vikundi 12 vya kwaya vilishiriki mashindano hayo na kwaya ya akina mama kutoka jimbo la Murongo kuibuka washindi.

Askofu wa KKKT Dayosisi ya Karagwe Mchg. Dakt. Benson Bagonza: Picha na Merabu Birakashekwa

Na Jovinus Ezekiel

Waumini wa kanisa la Kiinjili la kilutheri Tanzania Dayosisi ya Karagwe wametakiwa kuendelea kuamini imani yao kwa kujiepusha na imani ambazo zinaweza kuwapotosha katika suala la kumuamini Mungu.

Akitoa neno la Mungu kwa waumini wa kanisa hilo waliojumuika pamoja katika tamasha la nne la uimbaji la wanawake wa Dayosisi hiyo Septemba 15, 2023 kwa kuhusisha vikundi 12 vya kwaya ambayo vimeshiriki mashindano kwenye tamasha hilo, Askofu wa Dayosisi ya Karagwe Mchungaji Dkt Benson Bagonza amesema kuwa waumini wa dayosisi hiyo inabidi waendelee kumwamini Mungu katika imani yao.

“Waumini watakapoishi katika imani yao na kuacha imani ambazo zimelenga kuwaaminisha mambo ambayo Mwenyezi Mungu hayalengi kumwamini ikiwemo matumizi ya chumvi, mafuta, na matumizi ya maji kwani masuala hayo katika maandiko matakatifu hayakuelezwa kuwa ndio yatakayomukoa mwanadamu” Amesema Askofu Bagonza

Askofu Bagonza katika hatua nyingine amesema kuwa kwa sasa baadhi ya ndoa zimekuwa zikiishi bila amani kutokana na kutokuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu hali inayochangia kutoheshimiana baina ya mke na mume.

Naye  mratibu wa tamasha hilo la wakina mama mchungaji Elieth Kiiza mkuu wa idara ya wanawake, wanaume na watoto katika dayosisi ya Karagwe  amesema  kuwa kufanyika kwa matamasha haya kuna tija kubwa hasa kujenga imani kwa waumini katika kumwamini Mungu.

Baadhi ya waimbaji wa kwaya ya akina mama kutoka kanisa kuu Lukajange: Picha na Merabu Birakashekwa

Hata hivyo miongoni mwa kwaya 12 zilizoshiriki mashindano kwaya tatu zimepata ushindi ikiwemo kundi namba 6  kutoka jimbo la Murongo imepata ushindi wa kwanza , na kwaya kundi namba 2 ya jimbo la Ihembe imepata  ushindi wa pili na kwaya kundi 9  kutoka jimbo la Lukajange imeibuka na ushindi wa tatu.