Karagwe FM

Livingstone Byekwaso:Tokomezeni kwa vitendo unyanyapaa kwa wahanga wa marburg

10 June 2023, 10:53 am

Katibu mkuu wa shirika la Karagwe Media Association (KAMEA) linalomiliki Radio Karagwe mkoani Kagera Bw. Livingstone Byekwaso amewaasa wandishi wa habari mkoani hapa na wasanii wa fani mbalimbali kutekeleza kwa vitendo mipango yao ya kupambana na vitendo vya unyanyapaa na ubaguzi kwa wahanga wa ugonjwa wa marburg.

Bw. Byekwaso amesema hayo Juni 8 mwaka huu mjini Kayanga wilayani Karagwe wakati akifunga mafunzo ya siku moja kwa wandishi wa habari na wasanii wa majigambo mkoani Kagera yaliyofadhiliwa na shirika la kuhudumia watoto UNICEF na kuandaliwa na Radio Karagwe.

Katibu mkuu wa KAMEA Bw. Livingstone Byekwaso (kulia), Mkurugenzi wa Radio Karagwe Mch. Dkt. Godfrey Aligawesa (katikati) na Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe Dk. Agnes Mwaifuge.

Bw. Byekwaso pia ameonesha matumaini kuwa wandishi wanao uwezo wa kuponya vidonda vilivyoachwa na Marburg hasa kwa wakazi wa Bukoa vijijini.

Mwezeshaji katika mafunzo hayo mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe Dkt. Agnes Mwaifuge amevishukuru vyombo vya habari mkoani Kagera kwa kuelimisha jamii na kusaidia kuepusha maambukizi kuenea zaidi.

Amesema kuwa bila vyombo vya habari kutoa elimu watu wangeendekeza imani za kishirikina na wangepuuza tahadhari zinazoelekezwa hali ambayo ingesababisha vifo kuongezeka

Picha ya pamoja ya washiriki wa semina, waandaaji na mwezeshaji

Kwa upande wake mkurugenzi wa Radio Karagwe Mchungaji Dkt. Godfrey Aligawesa amewasisitiza wandishi wa habari kuendeleza elimu dhidi ya umuhimu wa jamii kurudi katika maisha yao ya kawaida kwa kushirikiana na waliopona marburg badala ya kuendelea kuwatenga. Ameshauri wandishi wa habari kuwa mfano kwa kutembelea baadhi ya familia zilizokuwa na wagonjwa wa marburg ili kuudhhirishia umma kwamba ugonjwa umekwisha.