Karagwe FM

Askofu atabaruku altare parokia ya Businde

18 September 2023, 2:19 pm

Askofu wa Jimbo Katoliki Kayanga, Mhashamu Almachius Rweyongeza (katikati) akionesha masalia ya Mt.Yohane Paulo II wakati wa misa ya uzinduzi wa jengo jipya la Parokia ya Businde: Picha na Eliud Henry

Na: Eliud Henry

Askofu wa Jimbo Katoliki Kayanga, Mhashamu Almachius Rweyongeza ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 163 wa Parokia ya Mtakatifu John Chrysostorm-Businde pamoja na kutabaruku altare ya parokia hiyo kwa kuzika masalia ya Mt.Yohane Paulo II kama ishara ya kutoka katika matumizi ya kawaida kwenda kwenye matumizi ya altare.

Maadhimisho hayo yamefanyika Septemba 17, 2023 katika parokiani Businde, ambapo pamoja na mambo mengine, Mhashamu Rweyongeza, amezindua jengo la parokia hiyo pamoja na kubariki vifaa kadhaa vya altare na kubariki jozi 5 za ndoa.

Askofu Almachius Vincent Rweyongeza akibariki na kuzindua kanisa la Mt Yohane Chrysostomo, Businde: Picha na Eliud Henry.

Akitoa homilia mbele ya waumini wa parokia hiyo amesisitiza juu ya faida za kusamehe akisema kukosea ni jambo la kibinadamu ila kusamehe ni jambo la ki-Mungu na kuongeza kuwa kusamehe ni kutakasa kumbukumbu.

Amewaasa waamini kuacha chuki, hasira, ubaya na wivu na kuwa wasiweke mipaka katika kusamehe.

Ameongeza kuwa, msamaha na huruma huleta amani hivyo waamini wamuige Mungu kupitia kwa mwanae Yesu Kristu aliyetamka maneno ya msamaha msalabani.

Katika tukio jingine, Mhashamu Rweyongeza, amekabidhi cheti cha shukrani kutoka Radio Maria Tanzania, kwa wana parokia ya Businde iliyoshika nafasi ya kwanza katika kampeni ya marathon 2023.

Mhashamu Baba Askofu wa Jimbo Katoliki Kayanga Almachius Vincent Rweyongeza akipanda mti wa kumbukumbu katika uzinduzi kanisa la Mt. Yohane Chrysostomo, Businde Jumapili, 17-9-2023: Picha na Eliud Henry