Karagwe FM

Bashungwa: Serikali inaendelea kuboresha maslahi ya walimu

27 October 2023, 9:14 pm

Waziri wa ujenzi na mbunge wa jimbo la Karagwe Innocent Bashungwa akiongea na wanachama wa CWT wilayani Karagwe katika kilele cha siku ya Mwalimu Duniani: Picha na Eliud Rwechungura

Na Jovinus Ezekiel

Waziri wa ujenzi na mbunge wa jimbo la Karagwe Innocent Bashungwa amewahakikishia walimu wa wilaya ya  Karagwe kuwafikishia changamoto zinazowakabili ikewemo madeni ya walimu na kikokotoo cha malipo ya  msitaafu kutokuwa rafiki kwa serikali ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.

“Niwaahidi tutaendelea kushirikiana, Jambo lenu ni Jambo la Serikali pia ni jambo langu mimi kama Mbunge wa Jimbo la Karagwe, vile vile niwaahidi wakati mtakapojiandaa kufanya Bonanza lenu, nitaleta vifaa vya michezo katika tarafa zote”

Amesema hayo tarehe 27 Oktoba 2023 wilayani Karagwe mkoani Kagera katika Sherehe ya kuadhimisha kilele cha siku ya Mwalimu Duniani na miaka 30 ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) yenye kauli mbiu “Walimu Tuwatakao, kwa Elimu Tuitakayo, Lazima Kutatua Uhaba wa Walimu”

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya mama yetu, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni sikivu imeendelea kulipa Madeni ya Watumishi ya Mishahara na yasiyo ya Mishahara kwa nyakati tofauti” amesema Bashungwa

Aidha, Bashungwa amesema tangu Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, Serikali imeajiri jumla ya walimu 29,879 wa Shule za Msingi na Sekondari nchini ambapo takwimu zinathibishisha Rais anavyothamini kada ya Walimu.

Bashungwa amemshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo tangu aingie halmashauri ya wilaya Karagwe imeshapokea Bilioni 3.113 kuboresha elimu ya msingi na Bilioni 5.514 kuboresha elimu ya Sekondari.

Wanachama wa CWT wilayani Karagwe katika kilele cha siku ya Mwalimu Duniani: Picha na Eliud Rwechungura

Kuhusu Kanuni ya Malipo ya Mkupuo na Malipo ya Pensheni kwa Wastaafu (Kikokotoo), amesema Serikali ya imeendelea kuwa sikivu na kuwathamini walimu wastaafu, na watumishi wote waliotumikia Taifa hili.

Kadhalika, Bashungwa amewapongeza Walimu wa kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na maarifa na amewasisitiza kuzingatia maadili ya kazi ya ualimu wakati wanapotekeleza majukumu yao

“Niwaahidi tutaendelea kushirikiana, Jambo lenu ni Jambo la Serikali pia ni jambo langu mimi kama Mbunge wa Jimbo la Karagwe, vile vile niwaahidi wakati mtakapojiandaa kufanya Bonanza lenu, nitaleta vifaa vya michezo katika tarafa zote”