Karagwe FM

Wanawake walia na mzigo wa kuhudumia familia bila malipo

25 April 2024, 10:25 pm

Baadhi ya wanawake wanaohudumia familia zao bila malipo wakiwa katika kongamano. Picha kwa msaada wa mtandao

Serikali ya Tanzania yakumbushwa kusimamia utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya wanawake na Jinsia ya mwaka 2000 ili kuwapunguzia wanawake mzigo wa kazi za huduma zisizokuwa na malipo.

Na. Edisoni Tumaini Galeba

Wakizungumza na makala haya kwa nyakati tofauti,akina mama wilayani Karagwe walisema kuwa, licha ya serikali kutungapitia  sera ya maendeleo ya wanawake na jinsia ya mwaka 2000,kuweka lengo la  kukuza haki na usawa wa kijinsia katika nyanja zote za maisha na maendeleo usawa wa  kijinsia,utekelezaji wa lengo hilo  umebaki kuwa changamoto katika familia nchini Tanzania.

Walisema kwamba wanawake wamekuwa wakilemewa na majukumu ya nyumbani huku wanaume wakitumia muda mchache kutekeleza majukumu ya utunzaji wa familia ikilinganishwa na wanawake.

Loveness Kashalazi mwanamke ambaye ni fundi cherehani katika kijiji cha Rukole wilayani Karagwe alisema kuwa,pamoja na kazi ya ushonaji,hulazimika kufunga mapema ofisi yake ili akabiliane na majukumu ya kuhudumia familia yake ambayo hayalipwi.

 “Serikali iangalie namna ya kuhakikisha kazi zisizokuwa na malipo zinathaminiwa ili kumweka mwanamke katika nafasi nzuri ya kushindana katika mzunguko wa kiuchumi na kijamii.”Alisema Loveness

Alizitaja kazi hizo kuwa ni pamoja na kufua,kufagia,kuosha vyombo,kusafisha watoto kutafuta kuni,kuchota maji nk.

Kwa upande wake Mastidia Kalungi Rushambila mwanamke mkazi wa mtaa wa Bomani katika mji wa Kayanga alisema kuwa,mwanamke pamoja na kufanya kazi nyingine,hulazimika kumhudumia pia mume wake kama wanavyohudumiwa watoto katika familia.

“Unapomwandaa baba ni sawa na kama unamwandaa mtoto wako,lazima ujue atakula nini, atavaa nini,atalala vipi, kazi ni nyingi sana. Kazi hizo Zingali kuwa na malipo, zingelikuwa zinainua uchumi kiasi Fulani kwenye familia.”Alisema Rushambila

Aliongeza kuwa,wanaume wanatakiwa kuthamini kazi za mama wa nyumbani anazozifanya kama zinavyothaminiwa kazi za utafutaji  wanazozifanya wanaume.

“Huwezi kumwambia baba kwamba ubaki nyumbani ulee familia na mimi niende nitafute. Atakwambia watoto siwawezi kubaki nao,hata kufagia nilishasahau kwani mara ya mwisho ni wakati nikiwa shule,na hata nikiwa shule nilikuwa nafua viatu vyangu tu na soksi za shule”.

Aliongeza kuwa ,muda umefika kwa wanafamilia kusaidiana kazi za nyumbani.Wakati mama aking’oa magugu kwenye mazingira,mwanaume anaweza kuwaosha watoto.

“Kazi za huduma zisizokuwa na malipo ndani ya familia zinasababisha mwanamke kujikita zaidi katika kazi hizo tu badala ya kwenda kufanya kazi nyingine zenye malipo ya moja kwa moja. Lakini ukithaminisha kazi za nyumbani zina mchango mkubwa katika uchumi wa familia”.

Bi.Farestina Anderson mwanamke katika kijiji cha Bwera A kata ya Igurwa alisema kwamba usawa wakati wa utekelezaji wa kazi zisizokuwa na malipo ni chachu ya maendeleo ya familia.

Alisema kuwa ,licha ya wanawake kubeba mzigo wa kazi za huduma zisizokuwa na malipo, hivi sasa akina mama wengi wamegeuka kuwa walezi wa familia kutokana na wanaume kusahau majukumu ya kuhudumia familia.

“Unakuta mama ananunua chumvi, chakula na matumizi mengine katika familia na hatimaye mama akichoka hukimbia familia na baba kwenda nje ya ndoa jambo linalowahangaisha watoto.”Alisema Bi.Anderson

Mchambuzi,mtafiti na Mwezeshaji wa maswala ya usawa wa kijinsia  ambaye pia ni mshauri katika Mtandao wa JInsia Tanzania TGNP Bwana Deogratias Temba alisema kuwa kazi zisizokuwa na malipo kuwaegemea wanawake hutokana na Mila na desturi , mazingira ya makuzi na malezi kuendekeza mfumo dume katika jamii.

“Kutokana na mila na desturi , makuzi na mazingira wanakolelewa watoto, mara nyingi kazi zisizokuwa na malipo zinaonekana kama ni za akina mama. Hata kama mwanaume hana kazi ya kufanya nyumbani , hawezi kusaidia hizi kazi”.  Ni tabia ambazo wanaume huzirithi kutoka kwa watu waliotangulia. Mtoto wa kiume akiona mama yake na dada yake ndio hufanya kazi hizo ,hukua akiona kuwa kazi hizo sio jukumu lake.Hata mwanamke aliyezoea kufanya kazi hizo,akiambiwa asifanye hujiona kama amenyanganywa majuku yake”.Alisema Temba.

Hata hivyo bwana Temba amesema kuwa, harakati za kuhamasisha mabadiliko katika mgawanyo wa majukumu wakati wa utekelezaji wa kazi za huduma zisizokuwa na malipo,hazina maana ya kuwalazimisha wanaume kufanya kazi hizo kwa nguvu,badala yake ni kuwahamasisha wanaume kuwatua wanawake mzigo mkubwa wa kazi hizi na hatimaye aweze kufanya majukumu mengine ya uzalishaji.

Afisa ustawi wa jamii halmashauri ya wilaya ya Karagwe Owokusima Kaihula alisema kuwa, ni muhimu wanaume watambue kuwa tayari Tanzania  inazitambua kazi zisizokuwa na malipo kiasi kwamba inapofika muda wa wanandoa kupeana talaka na uamuzi wa kugawana mali, Kazi za huduma zisizokuwa na malipo alizozifanya mwanamke ni kigezo cha kumpa haki ya kupata mgao wa mali.

“Utakuta akina mama wanatumia teknolojia za zamani,wakati mama anaendelea na kazi za huduma,mwanaume ni vema umsaidie mama kwa kumwekea teknolojia za kisasa za kurahisisha majukumu hayo.Mfano jiko la gesi badala ya kuni,kuvuta umeme kwa ajili ya kupikia pamoja na vifaa vya kurahisisha mapishi.”Alisema Kaihula

Ili kushughulikia uzito wa kazi kwa wanawake ncini Tanzania, Sera ya mwaka 2000 iliweka msisitizo katika:

Kuhakikisha kuwepo kwa mipango ya kitaifa ya kuwapunguzia wanawake uzito wa kazi,  kutoa elimu kwa jamii juu ya teknolojia mbalimbali zinazopatikana nchini,  kuwepo kwa utaratibu mzuri wa kupatikana, kusambaza na kutoa mafunzo kuzingatia uwezo na maumbile ya watumiaji,  kuimarisha huduma za jamii na vituo vya kulea watoto wadogo na huduma za afya,  teknolojia sahihi za kurahisisha upatikanaji na hifadhi ya maji na jamii ihamasishwe katika kushiriki kazi kulingana na uwezo wao ambazo zinafanywa na wanawake tu na matumizi ya nishati rahisi na nafuu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iitwayo” “kazi na ajira za utoaji huduma kwa ajili ya mustakhbali wa ajira zenye hadhi” inaonyesha kwamba wanawake wanatumia robo tatu zaidi ya muda wao katika kazi za kutoa huduma zisizo na ujira ikilinganishwa na wanaume na wanawake wengi ndio wanaofanya kazi za malipo za utoaji huduma.

Ripoti hiyo ambayo imependekeza hatua mbalimbali ikiwemo kuziba pengo la usawa katika ajira za malipo na zisizo na malipo, imetokana na takwimu zilizokusanywa kutoka nchi 64 zinazowakilisha theluthi mbili ya watu wote duniani walio na umri wa kufanya kazi , na imebainisha kwamba watu zaidi ya bilioni 2 walihitaji huduma mwaka 2015 wakiwemo watoto wa chini ya umri wa miaka 15 wapatao bilioni 1.9 na wazee milioni 200, na idadi hiyo inatarajiwa kufikia bilioni 2.3 mwaka 2030.