Karagwe FM

Neema kuwashukia wana KCU 1990 L.T.D

3 December 2021, 9:58 pm

Wajumbe wa bodi ya Chama Kikuu Cha Ushirika Kagera KCU 1990 LTD wamefanya mazungumzo na Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania Dr Benson Ndiege juu ya masoko ya zao la kahawa pamoja na mikakati uboreshaji wa shughuli za Ushirika zinazotekelezwa na Chama hicho.

Mazungumzo hayo yamefanyika jana jumatano katika Ofisi ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania TCDC ambapo pamoja na mambo mengine wajumbe wa bodi ya KCU wameeleza mikakati waliyonayo katika kuhakikisha wakulima wa zao la kahawa wanapata bei nzuri huku wakibainisha baadhi ya changamoto na vikwazo katika mnyororo wa thamani wa zao hilo.

Wajumbe wa Bodi ya KCU 1990 LTD wakiwa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania Dr. Benson Ndiege

Aidha wamesema kuwa wamejipanga ipasavyo kuhakikisha chama chao kinajiendesha kwakutegemea vitega uchumi vya chama hicho ambavyo ni ardhi,majengo na mali nyingine za Union

Kwa Upande wake Mrajis Dr Ndiege amepongeza mikakati mizuri ya Chama hicho katika kutafuta masoko ya kahawa nje ya Nchi “Tokeni nje wala msijifungie ndani tafuteni masoko ya kahawa,nendeni mkajifunze Nchi ya Uganda wamefanikiwaje kuwa na bei nzuri ya kahawa kwa mkulima” amesema Dr Ndiege

Ameishauri KCU kuanzisha shamba la mfano la kahawa litakalosaidia chama hicho kujiongezea mapato pamoja na wanachama kupata elimu ya kilimo bora cha kahawa kupitia shamba hilo.

Wajumbe wa Bodi ya KCU 1990 LTD wakiwa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania Dr. Benson Ndiege