Karagwe FM

Wakulima wa Kahawa Kyerwa wakombolewa na Juhudi AMCOS

25 April 2024, 10:13 pm

JUHUDI AMCOS  Ushirika wa Kilimo na Masoko umewapatia wakulima bei nzuri ya kihistoria.Wakulima sasa wanafaidika na zao la Kahawa wilayani Kyerwa Mkoani Kagera.

Na.Edisoni Tumaini Galeba

Ushirika wa JUHUDU ulioanzishwa rasmi mwaka 2012 na kuruhusiwa na Serikali  kusimama wenyewe mwaka 2018 umezidi kuongeza wigo wake kwa kuwaunganisha wakulima wa Wilaya za Karagwe na Kyerwa Mkoani Kagera kutoka wakulima 409 hadi 1209 mwaka huu.

Mwenyekiti wa Ushirika huo Donath Bishanga Emmanuel alisema kuwa ,msimu wa ukusanyaji wa Kahawa Chama hicho kimefanikiwa kuuza kahawa ya maganda jumla ya kg 1,912,726 na kupata kiasi cha Tanzania Shilingi 4,747,768,477.20.

“Tumefanikiwa  kuuza kahawa safi kwenye masoko ya Fair Trade jumla ya kg 653040 na kupata fedha ya premium kiasi cha USD 289,970.76 SWA NA Takriban Tanzania shilingi 681141315.24”. Alisema Emmanuel    

Mwenyekiti huyo alisema kuwa tayari wanaendelea kujenga kiwanda cha kukoboa Kahawa na tayari wamejenga ofisi ya kisasa iliyoghalimu kiashi cha Shilingi milioni 187,841,322.

Anastades Wilson ni mkulima  katika Kijiji cha Umoja  Kata ya Rwabwele wilayani Kyerwa.Anaisha na mmewe na watoto

“Tulikokuwa tukiuza awali tuliuza kwa shilingi 800 hadi 100 na hatukulipwa fedha zetu kwa muda muafaka. Hivi sasa ukweli fedha zetu zinapatikana kwa muda muafaka tunboresha familia zetu.”

Bi.Wilson aliongeza kusema kuwa, wanashuhudia maboresho ya mashamba yao kupitia elimu wanayopata kuhusu kilimo hai kinacholinda mazingira.

“Tunachimba mashimo kitaalam na kufukia makopo,tunatumia mbolea ya mboji, ukweli katika mazingira yetu tuko vizuri”. Alisema mkulima Anastades

Mkulima Wilson Gosbert Kanyirizi mme wake na Bi Anastades alisema kuwa , kupitia mafunzo ya kilimo bora yamewasaidia kufikia mafanikio makubwa ya kuwapeleka wanafunzi shule na kupata fedha za kulipia mahitaji ya shule kupitia JUHUDI AMCOS.

“Tulipojiunga na JUHUDI AMCOS kahawa yetu imepanda bei kutoka shilingi 1000 hadi zaidi ya shilingi 2000.”Alisema Kanyirizi

Imelda Chabukoba ( 75) ana mika 5 tangu ajiunge na Ushirika wa Juhudi AMCOS.Alisema kuwa Ushirika umemsaidia kuwasomesha wajukuu zake walioko Sekondari na mmoja Chuo kikuu.

“Kwa kweli sisi tunanufaika na Kahawa zetu.Kilo unazoziuza ndo fedha unazolipwa”Alisema Chabukoba.

Mzee mwingine ni Protase Kifafa(86) wa Kijiji cha Kalongo ,aliwahi kutumikia kifungo cha miaka mitano Gerezani kabla ya kurudi kuendelea na shughuli za kilimo cha Kahawa. Alisema kuwa amewahi kunufaika na  mkopo wa shingi Laki moja kutoka katika Ushirika huo fedha zilizomsaidia kulipia mahitaji ya mwanae anayesoma chuo.Anasema kuwa anajitahidi sana kufuata masharti ya Ushirika huo hasa hasa kuzingatia taratibu za kilimo hai.

“Siwezi kuuza Butura(kuuza kahawa zikiwa bado shambani) wala siwezi kutumia madawa wala mbolea zenye kemikali”Alisema Kifafa

Afisa Ushirika Halmashauri ya wilaya Kyerwa Godbless Barnaba Munuo alisema kuwa,mafanikio ya Ushirika huo ni kuuza Kahawa iliyoongezwa thamani tofauti na vyama vingine ambavyo vimekuwa vikiuza kahawa ghafi pamoja na uaminifu wa viongozi wanaoongoza AMCOS hiyo.

“Wamejenga imani kwa wakulima, wana masoko yao maalum ambayo huwapatia bei nzuri, na fedha yote inayopatikana huirudisha kwa wakulima na wakulima wameona tija tangu wajiunge na chama chao”.Alisema Munuo

Alisema kuwa changamoto ya soko la kahawa ni ubora wa zao hilo changamoto ambayo mara nyingi hushusha bei ya kahawa katika soko la Dunia.

“Kahawa bora inalipa. Kahawa haikuwahi kuwa na bei ndogo.Ninawasihi wakulima kuzingatia ubora wakulima watapata bei nzuri”.Aliongeza Munuo

Mwaka 2022 Waziri mkuu Kassim Majaliwa alitangaza Uamuzi wa Serikali wa kuondoa tozo 42 kati ya 47 walizokuwa wakitozwa wakulima wa kahawa Mkoani Kagera hadi kufikia tozo 5 unaonekana kuwanufaisha wakulima wa zao hilo wilayani Kyerwa Mkoani Kagera.

Tozo hizo zilizopungua kufikia  jumla ya Shilingi 267 kwa kila kilo ya kahawa, kutoka Shilingi 830 za awali umerudisha imani ya wakulima waliokuwa wameanza kukata tama kutokana na zao hilo kutowanufaisha wao moja kwa moja.

“Bei ya kahawa imeendelea kuimarika kwani katika msimu huu wakulima walilipwa shilingi elfu 1,300 kwa kilo moja ya kahawa ya maganda na Shilingi elfu 3,300 kwa kilo moja ya kahawa hai (Organic cofee).”

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema baadhi ya vyama vya ushirika vimekuwa vikiwaumiza wakulima wa kahawa kwa kuwaongezea tozo zisizokuwa na tija.

Awali AMCOS mkoani Kagera zilikuwa zikifanya kazi chini ya Vyama vikuu vya Ushirika na hazikuwa huru kukusanya wala kuuza Kahawa ya wanachama wake badala yake kazi hiyo ilikuwa ikifanywa na vyama vikuu vya Ushirika.