Karagwe FM

Wananchi Karagwe wamshukuru Rais Dkt. Samia kwa miradi ya maendeleo

6 July 2023, 8:51 pm

Baadhi ya wananchi wa kata ya Nyakakika wilayani Karagwe wakiwa kwenye mkutano wa mbunge na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Innocent Bashungwa. picha na Ospicia Didace

Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Karagwe mkoani Kagera wameishukuru serikali kwa kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

Na Ospicia Ddace

Wananchi wa wilaya Karagwe wameishukuru na kuipongeza serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miradi mikubwa ya maendeleo iliyojengwa na inayoendelea kutekelezwa ndani ya wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.

Salamu hizo zimetolewa na Wananchi kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya Mbunge Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ya kukagua miradi ya maendeleo na kuongea na wananchi wa kata za Bugene, Nyakakika, Igurwa na Kanoni.

Wananchi wamemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuridhia na kutoa shilingi bilioni 70 kwa ajili utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa Lwakajunju ambao tayari umeanza kutekelezwa.

Aidha, Wamemshukuru Rais Samia kwa kutoa shilingi bilioni 4 kujenga shule maalum ya Sayansi kwa Wasichana Kagera river katika eneo la Rwambaizi kata ya Kanoni ambayo ipo katika hatua za ukamilishaji ili kuanza kupokea wanafunzi kidato cha kwanza hadi kidato cha sita.

Katika Sekta ya Miundombinu, Wamemshukuru kwa Ujenzi wa barabara za lami zitakazofungua uchumi wa wilaya ambazo ni barabara ya Karagwe – Nyaishozi mpaka Benako inayoendela kujengwa kwa kiwango cha lami, barabara za Omugakorongo-Igurwa-Murongo ambayo ipo katika maandalizi ya kuanza utekelezaji.

Hali kadhalika, Barabara ya Omurushaka-Kaisho-Murongo ambayo ipo katika hatua za mwisho za kusaini mikataba na Kipande korofi cha barabara ya Nyakahanga-Bushangaro eneo la “Kujura Nkeito” kimewekwa lami na eneo korofi la “Bigoro” mkandarasi ataanza kazi ya ujenzi wa kilometa 2 za lami.

Vile vile, Wameshukuru kwa Ujenzi na ukamikishaji wa Hospitali ya Wilaya Karagwe inayoendelea kutoa huduma pamoja na ujenzi wa kituo cha afya cha Kibona kwa ajili ya tarafa ya Kituntu, ujenzi wa kituo cha afya katika tarafa ya Nyabiyonza utakaoanza katika bajeti ya mwaka huu wa 2023/24.

Mbunge wa jimbo la Karagwe na waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa Mhe.Innocent Bashungwa (aliyevaa shati la kitenge) akipunga mkono kwa wananchi wakati wa ziara yake jimboni, picha na Ospcia Didace

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa amewahakikishia Wananchi wa Jimbo la Karagwe kuwa Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwatumikia kwa jitihada kubwa na unyenyekevu mkubwa.