Karagwe FM

Rushwa, kuvuja siri chanzo cha uvunjifu wa amani Kagera

9 September 2024, 21:46

Bw. Jawadu Swaib Yusuph (aliyesimama) akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwasa. Picha na Theophilida Felician

Kipindi cha kuelekea chaguzi hapa nchini viongozi wa taasisi mbalimbali hujitokeza na kuiasa jamii juu ya umuhimu wa kuitunza amani ya nchi hasa kwa mikoa ya pembezoni ambayo kwa kiasi kikubwa inapakana na mataifa yenye ukosefu wa amani

Na Theophilida Felician.

Taasisi ya umoja wa amani kwanza mkoa wa Kagera imebaini kuwa changamoto ya rushwa, uvujishaji wa siri za viashiria vya uvunjifu wa amani pindi yanaporipotiwa kwa vyombo vya ulinzi na usalama.

Akiongea na viongozi na wanachama wa taasisi hiyo waliokutana katika kata Kibimba wilaya Ngara hivi karibuni kwa lengo la kuwapa mafunzo mabalozi wapya wa amani mwenyekiti wa umoja huo Maulid Rashid Kambuga akiungana na timu ya viongozi wenzake amesema kuwa lengo la umoja wa amani kwanza ni kuunga mkono juhudi za serikali katika kupambana na mambo yote yenye viashiria vya kuhatarisha amani kwa jamii na nchi kwa ujumla.

Mwenyekiti wa taasisi ya Amani Kwanza bw. Maulid Rashid Kambuga (aliyesimama). Picha na Theophilida Felician

Amesema changamoto ya rushwa imekuwa ni miongoni mwa matatizo yanayowaathiri walio wengi kupitia nyanja mbalimbali yakiwemo hata maeneo ya baadhi ya ofisi za umma jambo ambalo laweza kusababisha madhara iwapo halitoshughulikiwa katika kudhibitiwa.

Sauti ya Maulid Rashid Kambuga

Kwa upande wake katibu wa umoja huo Supery Balingilaki Jeremih ameyataja mafanikio katika utendaji kazi hasa hasa utatuzi wa migogoro, ya ardhi, ndoa, utumiaji mbovu wa madaraka pamoja na kufanikiwa kupunguza wimbi la akina dada waliokuwa wakikita kambi kwa ajili ya biashara ya ngono maeneo ya vituo vya magari, Rusumo, Kabanga, Benako, na Nyakahura tatizo ambalo kwa mjibu wa wataalamu wa afya ilionekana kuchochea kasi ya maambukizi ya magonjwa ya zinaa kwa wakazi wa maeneo tajwa.

Amewapongeza idara ya uhamiaji kwa kupambana hadi kupunguza adha hiyo kwani kwa sasa kuna nafuu na kuahidi kuwa taasisi hiyo itatembea mguu kwa mguu ili kuhakikisha elimu ya amani haimwachi mtu nyuma hususani katika kipindi hiki cha uchaguzi wa serikali za mitaa.

Mwakilishi wa waganga wa tiba asili mkoa wa Kagera bi Sunath Ayubu. Picha na Theophilida Felician

Katika mafunzo hayo wameshiriki makundi tofauti wakiwemo na waganga wa tiba asili ambapo Sunath Ayubu kwa niaba ya waganga wenzake amesema ni vyema elimu ya amani ikahamasishwa kwa kina katika jamii hali itakayosaidia kuyapunguza matukio ya uhalifu.

Hata hivyo mada nne (4) zimetolewa kwa walengwa ambazo ni kutoka Umoja wa amani kwanza, idara ya Uhamiaji, Takukuru na Usalama barabarani.

Kwa upande wao waratibu wa mafunzo ambao ni Msabila Raphaeli, Jastin Hassan Jackson wamesema kwamba mafunzo hayo yaliyozinduliwa Ngara yataenezwa ngazi ya kata, wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla kwakiwango cha ngazi ya cheti hadi diploma.

Naye mgeni rasmi kwa niaba ya mkuu wa mkoa Jawadu Swaibu Yusuph ambaye ni afisa tarafa ya Nyamiaga awali amepongeza jitihada za taasisi ya umoja wa amani kwanza kwa jinsi ilivyolivalia njuga suala la amini ambayo ni uhai wa kila kitu duniani kote.

Amekiri kuwepo kwa baadhi ya changamoto za viashiria vya uvunjivu wa amani kwa Kagera hususani matukio ya watu kujinyonga, kunyongwa, migogoro ya aridhi, mifugo yakigeni kutoka nchi za Rwanda, Uganda, Burundi, na uhamiaji haramu.

Sauti ya Mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Kagera ambaye ni afisa tarafa ya Nyamiaga wilaya ya Ngara bw.Jawadu Swaibu Yusuph

Kwa pamoja wameazimia mambo mbalimbali na muhimu yatakayotekelezwa katika shuguli za umoja huo.