Karagwe FM

Wananchi watakiwa kuepuka waganga wa tiba asili wasiosajiliwa

9 September 2025, 17:56

Katibu mkuu wa chama cha waganga wa tiba asili TAMESO (T) Lucas Mlipu (aliyesimama). Picha na Theophilida Felician

Wimbi la waganga wa tiba asili wasiosajliwa na baraza la tiba asili na tiba mbadala limezua hofu kwa chama cha waganga wa tiba asili TAMESO (T) na kutoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari

Na Theophilida Felician, Dodoma

Wananchi wanaotumia tiba asili na tiba mbadala nchini wametakiwa kuwa makini wanapokuwa na uhitaji wa huduma hiyo ili kuepuka madhara mbalimbali ya ukatili yakiwemo mauaji.

Ametoa kauli hiyo katibu mkuu wa chama cha waganga TAMESO (T) Bw Lukas Joseph Mlipu wakati akizungumza na Radio Karagwe makao makuu ya ofisi za chama hicho Dodoma na kuongeza kuwa kumekuwepo na matukio kadhaa ya kikatili wanayokumbana nayo wananchi yakihusisha huduma ya tiba asili.

Amefafanua kuwa matukio yanamna hiyo yanapotokea chama hicho katika ufuatiliaji wake mara kadhaa wamebaini kuwa watu wanaosababisha madhara siyo waganga halali bali baadhi yao wanatumia taaluma ya uganga kama kichaka cha kujificha na hatimaye kuendesha maovu yao kwa jamii.

Katibu huyo ametolea mfano wa tukio la hivi karibuni la mwananchi mmoja Juma Yoram Nyambihira aliyeuawa na mtu aliyejitambulisha kuwa mganga Ally Juma Shaban huko kitongoji cha makazi mapya wilaya ya Kibaha vijijini mkoa wa pwani.

Katibu mkuu wa chama cha waganga wa tiba asili TAMESO (T) Lucas Mlipu

Amebainisha baada ya tuikio hilo TAMESOT kupitia katibu wake mkoa wa Pwani Ally Masusa Ally wamefuatilia kwa ukaribu na kubaini kwamba Ally Juma hakuwa mganga bali akiwa anaishi maeneo hayo alijitambulisha kuwa ni mganga jambo ambao halikuwa na ukweli hivyo alionekana akijihusisha na shuguli za ukataji mkaa pamoja na marehemu Juma Yoram hadi umauti kumkuta.

Kufuatia tukio hilo na mengine ametoa wito akiwatahadharisha wananchi kuendelea kuwa makini na watu wanamna hiyo wanaoichafua tiba asili katika jamii huku akitoa pole kwa ndugu, jamaa na wananchi kwa ujumla kuondokewa na mpendwa wao.

Katibu mkuu wa chama cha waganga wa tiba asili TAMESO (T) Lucas Mlipu