Karagwe FM

Serikali kujenga mabweni mawili sekondari Bugene

20 April 2024, 1:59 pm

Shule ya sekondari Bugene wilayani Karagwe. Picha Na. Eliud Rwechungura

Licha ya jitihada kubwa za serikali kuboresha miundo mbinu, shule nyingi za msingi na sekondari za umma hukabiliwa na baadhi ya changamoto ambazo kila mara huziwasilisha kwa viongozi wanapopata fursa ya kufanya hivyo.

Na Ospicia Didace

Serikali imeahidi kujenga mabweni mawili pamoja na kukamilisha ujenzi wa bwalo katika shule ya sekondari Bugene wilayani Karagwe mkoani Kagera ili kuendelea kuboresha mazingira ya wanafunzi kujifunza

Akiwa katika mahafari ya 9 ya kidato cha sita katika shule ya sekondari ya Bugene kata ya Bugene wilayani Karagwe Aprili 19, 2024 Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa alisikia changamoto za shule hiyo kupitia risala ya wahitimu wa kidato cha sita iliyosomwa na mwanafunzi na Paula Alistides ikibainisha ukosefu wa bwalo la shule kwa ajili ya chakula na upungufu wa mabweni.

Sauti ya mhitimu katika risala bi Paula Alistides

Baada ya kusikia changamoto za shule hiyo waziri Bashungwa aliahidi kuchangia bati 519 huku akiongeza kuwa serikali itajenga mabweni mawili na kupiga simu kwa naibu katibu mkuu TAMISEMI (elimu) Dk Charles Msonde kupata ufafanuzi wa mchango wa serikali ambaye alikubali kuunga mkono juhudi za waziri Bashungwa.

Pia Dkt. Msonde amewapongeza wananchi kwa kujitoa na kuanza ujenzi wa bwalo kwa kujenga msingi na kumuagiza Mhandisi wa Halmashauri kufanya tathmini ya vifaa vinavyohitajika katika ujenzi ili Serikali iunge mkono jitihada za wananchi.

Sauti ya waziri Bashungwa na naibu katibu mkuu TAMISEMI (elimu) Dk. Msonde

Bashungwa amesema Shule ya Sekondari Bugene imekuwa ikifanya vizuri katika taaluma hivyo Serikali itahakikisha inaweka mazingira rafiki ya kujifunza na kufundishwa ili ufaulu uongezeke kimkoa na kitaifa.

Mbunge wa jimbo la Karagwe na waziri wa ujenzi Innocent Bashungwa (mwenye scarf) akiwa mgeni rasmi katika mahafali ya kidato cha sita Bugene sekondari

Shule ya sekondari Bugene yenye wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita ni shule kongwe na ambayo kwa kiasi kikubwa inatazamwa na halamashauri ya Karagwe kama kitovu cha elimu wilayani hapa