Karagwe FM
Karagwe FM
12 November 2026, 21:56

Shirika la kuhudumia watoto na vijana wenye ulemavu wilaya za Missenyi, Karagwe, Kyerwa na Ngara mkoani Kagera CBIDO limebaini pengo la elimu ya afya ya uzazi kwa kundi la vijana wenye ulemavu na kuanzisha kampeni ya elimu kwa ajili ya kundi hili kupitia mradi wake wa Pamoja unaotekelezwa katika wilaya hizo
Na mwandishi wetu, Missenyi-Kagera
Walimu na wauguzi wilayani Missenyi mkoani Kagera wametakiwa kutoa elimu juu ya afya ya uzazi kwa vijana ili kuwaepusha kujiingiza katika tabia hatarishi zinazosababisha kubeba ujauzito katika umri mdogo na ndoa za utotoni
Wito huo umetolewa na mtaalamu wa afya ya akili na mnasihi kutoka shirika la CBIDO linalohudumia watoto na vijana wenye ulemavu Bi Alice Alinda Kishweko wakati wa mafunzo kwa walimu na wauguzi juu ya masuala ya afya ya uzazi kwa vijana

Kwa upande wake Bwana James Mongi kutoka shirika la CBIDO amesema kuwa kupitia mradi wa “Pamoja Programu” wamewajengea uwezo walimu na wauguzi kutoka vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya ili wasaidie kuimarisha eneo la ulinzi na usalama wa mtoto na watu wengine wenye ulemavu
Kwa upande wake muuguzi mkuu wa wilaya ya Missenyi Bi Lucy Eustace ameishauri jamii kuhakikisha vijana wenye ulemavu na walioko katika umri wa kubalehe wanapata mahitaji ya Msingi ikiwemo huduma ya afya ya uzazi kama inavyofanywa kwa makundi mengine

Washiriki wa mafunzo wamesema kuwa elimu waliyopata wataitumia vizuri ili isaidie kupunguza masuala ya ukatili wa kijinsia pamoja na mimba za utotoni