Karagwe FM
Karagwe FM
18 September 2026, 20:02

Tatizo la upungufu wa madawati limekuwa likijitokeza kote nchini kila mwaka hasa nyakati za uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali na la kwanza kwa shule za msingi sambamba na uandikishaji wa kidato cha kwanza kwa shule za sekondari.
Na Mwandishi wetu, Missenyi
Kikundi cha mtandaoni (WhatsApp) cha Missenyi na Maendeleo kimekabidhi mchango wa madawati 85 yenye thamani ya shilingi milioni 5.1 kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Missenyi
Madawati hayo yamekabidhiwa Septemba 17.2026 baada ya kuchangwa na wanagroup wazalendo wa kikundi cha mtandao wa WhatsApp cha Missenyi na Maendeleo ili kupunguza tatizo la upungufu wa madawati katika shule za msingi na sekondari wilayani humo
Mgeni rasmi katika hafla ya kukabidhi madawati hayo amekuwa mkuu wa wilaya ya Missenyi Kanali Mstaafu Hamis Mayamba Maiga akishuhudia shule nne za msingi zikipata mgao wa madawati 85 kama zilivyotajwa na kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Missenyi Seraphina Rwegasira

Mratibu na kiongozi wa kikundi hicho bw. Respicius John amesema kuwa kikundi hicho kilianzishwa Agosti 21. 2020 kikihusisha wadau wa maendeleo na kwamba wazo la uchangiaji madawati lilianzishwa mwaka huu na mmoja wa wadau hao kisha utafiti ukabaini uhitaji wa kutekeleza jambo hilo kupitia michango ya hiari
Amesema kuwa kipaumbele cha mgao wa madawati umezingatia shule zilizokuwa na uhitaji mkubwa wa samani hizo huku akitaja mikakati ya kikundi hicho kwa siku zijazo
Naye mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Missenyi Kanali mstaafu Hamis Maiga ameitaka jamii ya Missenyi kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wadau hao huku akiwataka walimu wa shule zilizonufaika kutunza samani walizozipokea
Pia amewaagiza walimu wakuu kuanzisha utaratibu na ratiba ya kurekebisha samani zinazoharibika ili kuzuia upungufu mkubwa wa madawati shuleni

Hata hivyo kwa mujibu wa kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo bado kuna upungufu wa madawati 1,916
Ameiomba jamii na wadau wa maendeleo kuendelea na juhudi za uchangiaji wa madawati ili kumaliza kabisa tatizo la upungufu na kuweka mazingira bora ya wanafunzi kujifunza