

15 March 2025, 1:29 pm
Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Afya nchini Mh. Jenista Mhagama imetangaza kufanikiwa kuudhibiti ugonjwa wa marburg, ambao ulitangazwa kuibuka nchini mwezi Januari 2025 katika halmashauri ya wilaya ya Bihalamulo mkoani Kagera.
Na,Elisha Magege
Kufuatia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya kutangaza kufanikiwa kuuondoa ugonjwa wa homa ya marburg nchini, wananchi wilayani Sengerema wameipongeza Radio Sengerema kwa kushirikiana na serikali kutoa elimu juu ya ugonjwa huo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kutoka maeneo mbalimbali wananchi hao wamesema kupitia radio Sengerema wamepata elimu ya kujikinga na marburg jambo lililopelekea ugonjwa huo kuishia mkoani Kagera pekee.
Kufuatia pongezi hizo mratibu wa kituo cha habari na mawasiliano Sengerema Telecentre Bwn. Peter Marlessa amewashukuru wananchi wilayani hapo kwa kuendelea kuiamini radio yao huku akiahidi kuwa wataendelea kutoa elimu juu masuala mbalimbali yanayoihusu jamii.
Mbali na pongezi hizo wananchi pia wameiomba serikali kuendelea kutoa elimu za magonjwa mbalimbali ya mlipuko, ikiwemo ugonjwa wa M-POX ulioripotiwa kutokea nchini.
Hata hivyo taarifa iliyotolewa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama tar 13 Machi 2025 imesema Tanzania imefanikiwa kuudhibiti ugonjwa wa mlipuko wa marburg kutokana na kutokuwepo kwa mgonjwa mwingine yeyote tangu mgonjwa wa mwisho alipopatikana tarehe 28 Januari, 2025 na hadi kufikia tarehe 11 Machi, 2025 siku 42 zimepita.