Sengerema FM
Sengerema FM
28 February 2025, 11:07 am

Hakimu Kisoka ametoa hukumu kwa mshitakiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.
Na,Emmanuel Twimanye
Mahakama ya wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza imemhukuma Slyvester Elias (29) Mkazi wa Kijiji cha Nyehunge, Wilayani humo kwenda jela miaka 30 baada ya kukutwa na hatia ya kumlawiti binti wa miaka 10 .
Hukumu hiyo ya kesi ya Jinai namba 8399/2024 imesomwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Sengerema, Evod Kisoka mbele ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali Nyamhanga Tissoro.
Awali, Mwendesha Mashtaka aliieleza Mahakama kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo March,18, 2024, katika Kijiji cha Nyehunge wilaya ya Sengerema, mkoa wa Mwanza kinyume na vifungu vya 154(1)(a) pamoja na kifungu cha (2) cha sheria ya kanuni ya Adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.
Mshtakiwa alifikishwa Mahakamani kwa mara ya kwanza tarehe 29.07.2024 na kusomewa shtaka hilo ambapo alikana.
Upande wa Jamhuri ulileta mashahidi na shauri lilianza kusikilizwa katika mahakama hiyo April ,04 2024 na kuendelea hadi Januari 28, ambapo mshitakiwa alijitetea huku akikanusha vikali kutenda kosa hilo.
Baada ya Mahakama kupitia vifungu vya sheria na ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamhuri ikiwemo ripoti ya Mganga aliyemfanyia uchunguzi mtoto huyo, pamoja na cheti cha kuzaliwa cha mhanga, Mahakama imejiridhisha kuwa upande wa Jamhuri wameweza kuthibitisha shitaka bila ya kuacha shaka kwamba mtuhumiwa alitenda kosa hilo.
Baada ya kutiwa hatiani mshtakiwa aliiomba Mahakama imuachilie huru kwa kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na kudai kuwa alipitiwa na shetani.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu, Kisoka alimuhukumu mshtakiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela ili iwe fundisho kwa watu wengine.