Waziri Ndumbaro aweka jiwe la msingi ujenzi wa uwanja wa michezo Sengerema
3 July 2024, 8:12 pm
Waziri Dkt. Ndumbaro pia ametembelea shule ya Sengerema Sekondari ambapo Serkali imepanga kujenga miundombinu mbalimbali ya michezo,kwani Shule hiyo ni miongoni mwa shule 56 za michezo zitakazojengwa nchini.
Na;Elisha Magege
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Daniel Ndumbaro, ameweka jiwe la Msingi wa ujenzi wa Uwanja wa Mnadani uliopo mjini Sengerema na kuubadili jina kuwa uwanja wa Tabasamu kutokana na mchango mkubwa wa Mbunge wa Jimbo la Sengerema .
Akiongea katika hafla ya uwekaji jiwe la Msingi iliyofanyika uwanjani hapo Mhe. Dkt. Ndumbaro amesema kupitia juhudi za Mbunge, Halmashauri na wadau wengine ni vyema uwanja huo ukapewa jina la Tabasamu kwani amekuwa mstari wa mbele katika ujenzi wa uwanja huo na ametumia fedha za mfuko wa jimbo pamoja na mchango wake binafsi kufanikisha ujenzi wa uwanja huo, huku akimwagiza Mkurugenzi Mtendaji kuandaa andiko la maombi ya fedha za kukamilisha uwanja huo na kuyawasilisha Wizarani.
Mbunge wa Jimbo la Sengerema Mhe. Hamis Tabasamu amesema ujenzi wa uwanja huo kwa awamu ya kwanza ulianza tarehe 1 Aprili, 2024 na unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 360 ambapo ujenzi umefikia asilimia 75.
Aidha mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sengerema, Ndg. Mark Agustine Makoye amesema ujenzi wa uwanja wa michezo katika mji wa Sengerema ni hitaji la muda mrefu kwa wananchi hivyo amewaomba wananchi wa Sengerema kuwa tayari kuutumia uwanja huo kuibua vipaji vingi vya wanamichezo.