Orkonerei FM

Simanjiro Yapitisha Makadirio ya Bajeti ya Sh45 Bilioni kwa Mwaka 2026/27

15 February 2026, 5:46 am

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mhe Kaleya Melita Mollel (aliyesimama), Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe Mwanjaa Jacob na Kaimu DED Simanjiro Dominica Ngaleka (aliyevaa Miwani) wakifuatikia kikao cha mpango wa bajeti (Picha na Joseph Lyimo)

Baraza la Madiwani Simanjiro lapitisha rasimu ya bajeti ya Sh45.1 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/2027 katika bajeti hiyo,Sekta za Elimu, Afya, Kilimo, na Mifugo zimepewa kipaumbele.

Na Mwandishi Wetu

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, limeidhinisha rasimu ya mpango wa bajeti ya kiasi cha shilingi 45,136,269,016.60 kwa ajili ya mwaka wa fedha 2026/2027,ikiwa na lenga la kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Akiwasilisha rasimu hiyo mbele ya Baraza la Madiwani Jumamosi, Februari 14, 2026, Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Simanjiro, Happy Masatu, ameeleza kuwa maandalizi ya mpango huo yamezingatia miongozo ya serikali, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), pamoja na vipaumbele vilivyoibuliwa na halmashauri kulingana na mahitaji ya jamii.

“Mpango huu umelenga mwongozo wa maandalizi ya bajeti ya Serikali, hotuba ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati akifungua Bunge la 13, na vipaumbele vya halmashauri yetu,” amesema Masatu.

Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Simanjiro, Happy Masatu, akiwasilisha rasimu ya bajeti katika baraza la Madiwani halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro.

Amebainisha kuwa vipaumbele vikuu vitakuwa ni uboreshaji wa sekta ya elimu, afya, kilimo, na mifugo, huku mapato ya ndani yakitarajiwa kuongezeka kupitia ushuru wa madini, mazao, minada, na kodi za huduma.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mhe. Kaleiya Melita Mollel, amewataka madiwani na watumishi kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha fedha zinazotengwa zinaleta tija.

“Watu kule kwenye kata zetu wana matarajio makubwa katika kupata huduma muhimu kupitia bajeti ya mwaka huu kwenye sekta ya afya, elimu, maji, na miundombinu ya barabara,” alisisitiza Mhe. Mollel.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Simanjiro, Dominika Ngaleka, amewahakikishia madiwani kuwa usimamizi wa bajeti hiyo utafanyika kwa uadilifu mkubwa.

Amesema ushirikiano wa karibu kati ya watendaji na viongozi wa wananchi ndio utakaohakikisha miradi yote iliyopangwa inakamilika kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa.

Baadhi ya madiwani waonyesha matumaini makubwa na bajeti hiyo.

Diwani wa Mirerani, Salome Mnyawi, amepongeza mpango huo akisema utasaidia kukamilisha miundombinu muhimu ya afya katika mji wa Mirerani, huku Diwani wa Endiamtu, Lucas Zacharia, akieleza kuwa kuimarishwa kwa soko la madini (Tanzanite City) kutafungua fursa zaidi za kibiashara na kuongeza mapato ya wilaya hiyo.