Utumiaji wa ugoro chanzo kansa ya mdomo kwa vijana
23 April 2024, 7:57 pm
Kufatia kuwepo na wimbi kubwa la vijana nchini kujihusisha na utumiaji wa madawa ya kulevya ikiwemo ugoro, jamii imeonywa kuachana na matumizi ya madawa hayo ili kuondokana na madhara yanayoweza kumpata ikiwemo kupata kansa.
Na:Emmanuel Twimanye
Vijana Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza wametakiwa kuachana na matumizi ya ugoro ili kuepuka kukumbwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo kansa ya mdomo.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dkt Omary Sukari wakati akizungumza na radio Sengerema , kufuatia kuwepo kwa wimbi kubwa la vijana wanaojihusisha na matumizi ya ugoro.
Amebainisha kuwa ugoro una madhara makubwa ikiwemo kusababisha magonjwa mbalimbali kama kansa ya mdomo, koo na kongosho hivyo ni vyema vijana wakaachana na matumizi hayo ya ugoro.
Naye mmoja kati ya wauzaji wa ugoro Wilayani Sengerema amesema kuwa pamoja na kuyauzia makundi mengine bidhaa hiyo lakini wateja wake wakuu kwa sasa ni vijana wa kike na kiume.
Nao baadhi ya wananchi wameshangazwa na kitendo cha baadhi ya vijana katika kipindi hiki kutumia ugoro kwa kuwa jambo hilo lilikiwa limezoeleka kwa wazee.
Kwa uapande wao baadhi ya vijana wanaotumia ugoro walipotafutwa na Radio Sengerema kwa ajaili ya kuzungumzia suala hilo hawakutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari.
Aidha kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani WHO zinaonyesha utumiaji wa bidhaa za Tumbaku husababisha vifo kwa karibu nusu ya watumiaji wake na zaidi ya watu takribani Milioni 8 hufariki kila mwaka kutokana na matumizi ya Tumbaku.