Marufu pikipiki za Samia kuendeshea bodaboda
19 April 2024, 11:37 am
Chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Sengerema kimegawa pikipiki kwa viongozi wake wa kata na matawi ili kuwarahisishia kazi zao za kichama.
Na:Emmanuel Twimanye
Viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza waliopatiwa pikipiki na chama hicho wamepigwa marufuku kuzitumia pikipiki hizo kufanya Bodaboda.
Agizo hilo limetolewa na katibu wa Umoja wa wanawake (UWT ) Wilayani Sengerema Rosemary Mwakisalu wakati akitoa salamu za Jumuiya ya umoja huo katika mafunzo ya usalama barabarani kwa viongozi wa chama hicho waliopatiwa pikipiki na chama cha mapinduzi.
Amesema kuwa Pikipiki hizo zimetolewa na mweneyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) Taifa Mh, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi kwa viongozi wa chama hicho hususani makatibu na si vinginevyo.
Mkurugenzi wa Chuo cha Udereva Muungano Sengerema Donald Ngadaya amesema kuwa viongozi hao waliopewa pikipiki walikuwa hawana uelewa kuhusiana na masuala ya sheria na alama za barabarani ambapo tayari wamewafundisha na kuelewa huku akitarajiwa watakuwa maderreva bora
Naye Mkuu wa usalama barabarani Wilayani Sengerema Hamis Wembo amewataka madereva hao kwenda kuwa mabalozi kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani kutokana na mafunzo waliyoyapata.
Nao baadhi ya viongozi waliopata fursa ya mafunzo hayo wameahidi kutokwenda kuzitumia pikipiki hizo kwa shughuli za bodaboda huku wakiahidi kwenda kuzingatia mafunzo hayo ili kuepuka ajali za barabarani.
Ikumbukwe kuwa hivi karibuni Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Mh,Dkt Samia Suluhu Hassan alitoa pikipiki kwa viongozi wa chama cha mapinduzi Hususani makatibu ili kurahisisha utendaji kazi wa shughuli za cha hicho.