Sengerema FM
Sengerema FM
31 March 2026, 8:05 pm

Kufuatia kukithili kwa matukio ya wizi wa watoto wilayani Sengerema,Mahakama wilayani humo imemhukumu binti na mkazi wa buchosa kifungo cha mwaka mmoja jera ili iwe fundisho kwa watu wengine.
Na,Emmanuel Twimanye
Mahakama ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza imemhukumu Novina Yoel Kuboja (23), mkazi wa Buchosa wilayani humo, kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kosa la kuiba mtoto wa kiume mwenye umri wa miezi mitatu.
Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Evod Kisoka, ambapo mshtakiwa hakutaka kuisumbua mahakama kwa kukiri kutenda kosa hilo na kupatikana na hatia ya kuiba mtoto kinyume na kifungu cha 169 (1)(a) cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marejeo ya 2023.
Kwa mara ya kwanza, Novina amefikishwa Mahakamani Machi 30, 2026, na kusomewa shtaka linalomkabili na Wakili wa Serikali, Rivana Kasinisala, katika kesi ya jinai namba 6895/2026.
Inadaiwa alitenda kosa hilo mnamo Machi 11, 2026, katika kijiji cha Nyamatemele, kata ya Nyehunge, wilaya ya Sengerema.
Katika utetezi wake, mshtakiwa alieleza mahakama kuwa aliiba mtoto huyo kwa lengo la kwenda kumlea kwani yeye hana uwezo wa kupata mtoto.
Kauli hiyo ilipingwa vikali na upande wa mashtaka ambapo Wakili Kasinisala alisisitiza kuwa kitendo kilichofanywa na mshtakiwa ni cha kikatili na kinyume cha sheria, hivyo akaiomba mahakama itumie mamlaka yake kutoa adhabu kali ili kukomesha vitendo vya wizi wa watoto.
Akitoa hukumu hiyo, Kisoka amesema mahakama haina mbadala wa kutoa adhabu nyingine kwani kifungu husika kinatoa adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela, hivyo akaamuru mshtakiwa kutumikia kifungo hicho gerezani.
Hata hivyo muda mfupi baada ya mahakama kutoa hukumu hiyo baadhi ya wananchi wametoa maoni yao kuhusiana na hukumu hiyo nje ya viunga vya mahakama.