Sengerema FM
Sengerema FM
16 August 2025, 7:54 pm

Licha ya kuwa na mradi mkubwa wa maji wenye thamani zaidi ya Tsh.Bil 22 Wilaya ya Sengerema imekuwa na changamoto ya kukosa maji mara kwa mara hasa kwenye maeneo ya miinuko bila kutolewa ufafanuzi kwa wananchi.
Na,Peter Marlesa
Wananchi Wilayani Sengerema mkoani Mwanza Wameitaka mamlaka ya maji na usafi wa mazingira (Seuwasa)kufanya maboresho ili maeneo ya miinuko yafikiwe na huduma ya maji muda wote.
Hayo yanajili baada ya wananchi kuilalamikia mamlaka hiyo kuwa maeneo hasa yenye miinuko hukaa muda mrefu bila huduma ya maji,na kwamba mgao usio na ratiba maalumu unapunguza ufanisi wa huduma hiyo muhimu katika jamii.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa mamlaka ya maji Sengerema ,Mhandisi Sadala Khamis Sadick amesema kuwa changamoto za kijiografia ndio chanzo cha upungufu wa maji kwa baadhi ya maeneo mjini Sengerema, pamoja na hayo amewataka wananchi kulipia huduma hiyo kadri ya matumizi yao kwa wakati.
Mbali na changamoto hizo,Seuwasa imepiga hatua kubwa ya kutandaza mfumo wa maji,ambapo kwa mjini ni zaidi ya asilimia ya tisini na vijijini zadi ya asilimia 70 kwa wilaya yote.