Sengerema FM

PM Majaliwa: Walioiba vifaa tiba wachukuliwe hatua kali

19 May 2025, 8:40 pm

Waziri mkuu akizungumza na wananchi mjini Sengerema wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani hapo.Picha na Elisha Magege

Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa mkoa wa Mwanza uhakikishe unakamilisha uchunguzi wa watumishi wa Hospitali ya wilaya ya Sengerema wanaodaiwa kuhusika na wizi wa vifaa hospitalini hapo ili watakaothibitika wachukuliwe hatua za kisheria.

Waziri mkuu akiweka jiwe la msingi Hospitali ya wilaya ya Sengerema wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani hapo.Picha na Elisha Magege

Waziri mkuu Kassimu Majaliwa amefanya Ziara ya siku mbili katika Mkoa wa Mwanza akiwa wilayani Sengerema amekutana na sakata la wizi wa vifaa tiba lililotokea katika Hospitali ya wilaya Mwabaruhi na kuagiza wahusika kuchukuliwa hatua kali.

Na,Elisha Magege

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumatatu, Mei 19, 2025) wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi Hospitali ya wilaya ya Sengerema akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza, ambapo amewasisitiza watumishi kuwahudumia wananchi ipasavyo.

Waziri mkuu Kassimu Majaliwa akizungumzia tukio la wizi wa vifaa tiba Sengerema

Aidha mkuu wa mkoa wa Mwanza Mh. Said Mtanda amesema hatua zimeshaanza kuchukuliwa kwa walio husika na wizi huo ambapo tayali wameshakamatwa na jeshi la polisi,huku akisema pia uongozi wa mkoa ubaini changamoto kubwa katika hospitali hiyo ni udhaifu wa uongozi uliopo.

Sauti ya mkuu wa mkoa wa Mwanza Mh. Said Mtanda akizungumzia hatua walizochukua kwa walioiba vifaa tiba

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Dkt. Darison Andrew amesema pamoja na kutokea kwa changamoto hiyo , hospitali pia imepokea vifaa tiba mbalimbali toka Serikalini vyenye thamani ya shilingi milioni 418 ambavyo vinatumika kutolea huduma kwa wananchi.

Sauti ya DMO Sengerema Dkt. Darison Andrew akizungumzia sakata la wizi vifaa tiba Sengerema

Ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Sengerema ulianza kutekelezwa mwaka 2020, ambapo umekuwa ukitekelezwa kwa awamu na tarehe 16 August, 2023 ilianza kutoa huduma huku ujenzi huo ukiendelea na hadi kukamilika unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 3.1, ambapo mbali na Serikali kutoa fedha za ujenzi pia ilitoa shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.

Jengo la utawala Halmashauri ya Sengerema. Picha na Elisha Magege