

25 March 2025, 8:58 pm
Kwa sasa sehemu ya barabara ya ushoroba wa ziwa Victoria kutoka Sirari mpani mwa Tanzania na Kenya na Mtukula mpakani mwa Tanzania na Uganda imepita eneo la Kigongo Busisi ambapo imeunganishwa kwa kutumia vivuko vikubwa vitatu vya MV Mwanza, MV Misungwi na MV Sengerema.
Na,Elisha Magege
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imetembelea mradi wa ujenzi wa daraja la JP Magufuli (Kigongo-Busisi) lililopo Mkoa wa Mwanza. Daraja hili, linalounganisha mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani, lina urefu wa takriban kilometa 3.2 na linatarajiwa kubadili maisha ya wananchi.
Akizungumza mara baada ya kutembelea na kukagua daraja hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya PIC, Mheshimiwa Augustine Vuma, amesema kuwa mradi wa daraja hilo una thamani ya bilioni 610 na umefikia asilimia 97.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Dkt. Charles Msonde amesema daraja la J.P Magufuli (Kigongo Busisi)KM 3 litaanza kutumika rasmi Aprili 30 mwaka huu.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Ambrose Pascal, amethibitisha kuwa daraja limefika hatua za mwisho na kuwa katikati ya mwezi Aprili 2025, magari yataanza kupita.
Daraja hilo limejengwa kwa lengo la kuunganisha Barabara Kuu ya Usagara – Sengerema Geita KM90 ambayo ni sehemu ya barabara iliyopo kwenye Ushoroba wa Ziwa Victoria inayoanzia Sirari mpakani mwa Tanzania na Kenya hadi Mutukula mpakani mwa Tanzania na Uganda