Sengerema FM

Shehena ya viti vya meli ya Mv.Mwanza hapa kazi tu yawasili jijini Mwanza

25 March 2025, 8:23 pm

Mkuu wa Wilaya  Nyamagana Mhe. Amina Makilagi akifungua moja ya makontena yaliyo sheheni viti vya meli ya mv.Mwanza hapa kazi tu. Picha na Elisha Magege


Ujenzi wa meli kubwa zaidi ndani ya Ziwa Victoria itakayofanya safari zake kati ya Bandari ya Mwanza Kaskazini, Kemondo, Kenya na Uganda, umefikia asilimia 96 huku ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20 na magari makubwa 3.

Na,Elisha Magege

Mkuu wa Wilaya  Nyamagana Mhe. Amina Makilagi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ameongoza hafla fupi ya mapokezi ya magari tisa yaliyobeba makasha yenye mzigo wa samani zitakazofungwa kwenye Meli ya Mv. Mwanza inayojengwa katika ziwa Viktoria.

Akizungumza katika mapokezi hayo Mhe. Makilagi amesema kuwasili kwa samani hizo ni hatua muhimu katika kuelekea kukamilisha mradi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 96 ya utekelezaji wake na ambao unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Mei, 2025.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya  Nyamagana Mhe. Amina Makilagi akizungumza kwa niaba ya Rc Mwanza

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa TASHICO Bi. Amina Mtibampema amesema wamepokea vifaa yaani viti vya madaraja yote ambapo mara baada ya kukamilika kwa zoezi la umaliziaji wa meli hiyo kampuni hiyo ya meli itakwenda kufungua uchumi wa Mkoa, wafanyakazi wa TASHICO pamoja na Taifa kiujumla.

Sauti ya Kaimu Mkurugenzi wa TASHICO Bi. Amina Mtibampema akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa meli ya Mv.Mwanza

Mradi huo wa Meli ya Mv. Mwanza kwa sasa umefika asilimia 96 na fedha zilizolipwa hadi sasa ni asilimia 93. Aidha Meli hiyo itakapokamilika itakuwa ndiyo meli kubwa kuliko zote katika Ziwa Viktoria ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20 na magari makubwa 3.