

21 March 2025, 7:07 am
Matukio ya ubakaji wilayani Sengerema yanazidi kushamiri ambapo taarifa inayozungumzwa ni ya mtoto mwenye umri wa miaka 10 anayedaiwa kubakwa na watu wawili kwa nyakati tofauti.
Na,Emmanuel Twimanye
Jeshi la Polisi Wilayani Sengerema mkoani Mwanza linawashikilia watu wawili akiwemo mwalimu wa shule ya msingi Daud Ochieng (37) na Adon Sospeter (53) wakazi wa kata ya Ibisabageni kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi (10) wa shule ya msingi Bukala wilayani Sengerema kwa nyakati tofauti .
Akizungumzia tukio hilo mtoto aliyedaiwa kubakwa akiwa amelazwa katika Hospitali teule ya Wilaya ya Sengerema amekiri kubakwa na watu hao kwa nyakati tofauti .
Mama mzazi wa mtoto huyo amesikitishwa na tukio hilo na kueleza kuwa baada ya kugundua afya ya mtoto wake imedhoofika ndipo aliamua kumpeleka Hospitalini kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu ambapo uchunguzi huo ulibaini kuwa amebakwa.
Baba mzazi wa mtoto huyo amesema kuwa taarifa za kubakwa mtoto wake alipata akiwa kazini baada ya kupigiwa simu na mke wake na kumshauri kumpeleka Hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu .
Kufuatia tukio hilo Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi (CCM) na Katibu wa umoja wa wanawake (UWT) Wilayani Sengerema wamefika katika Hospitali teule ya Wilaya hiyo kumjulia hali mtoto huyo na kuomba sheria kuchukua mkondo wake dhidi ya watuhumiwa wanaodaiwa kufanya kitendo hicho.
Naye kamanda wa polisi Mkoani Mwanza Wibroad Mtafungwa amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa wote wawili na wapo mahabusu katika kituo cha Polisi Wilayani Sengerema na kwamba watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria mara baada ya uchunguzi wa tukio hilo utakapokamilika .