Sengerema FM

Mzee Lucas ahukumiwa kwa kumbaka mjukuu wake wa miaka 13

14 March 2025, 8:02 pm

Lucas Maselele (56) akiwa chini ya ulinzi wa jeshi la polisi baada ya kuhukumiwa miaka 30 jela. Picha na Emmanuel Twimanye

Matukio ya ubakaji nchini yanazidi kushika kasi ambapo mzee mmoja mwenye umri wa miaka 56 amehukumiwa miaka 30 kwa kosa la kumbaka mjukuu wake wa miaka 13, baada ya mke wake kusafiri.

Na,Emmanuel Twimanye

Mahakama ya Wilaya Sengerema Mkoani Mwanza  imemuhukumu Lucas Maselele (56), mkazi wa kijiji cha Lugata kwenda jela miaka 30 baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mjukuu wake (13).

Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Sengerema, Evod Kisoka Katika kesi hiyo ya Jinai namba 16492/2024.   

Awali, Mwendesha Mashtaka wakili wa Serikali Nyamhanga Tissoro aliieleza Mahakama kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo Juni 04, 2024, katika Kijiji cha Lugata, wilaya ya Sengerema kwa kumbaka mjukuu wake wakati mke wake ameenda msibani mpaka alipofumaniwa na mke wake akifanya kitendo hicho kinyume na vifungu vya 130(1)(2)(e) pamoja na kifungu cha 131(1) vya sheria ya kanuni ya Adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.

Mshtakiwa alifikishwa mahakamani kwa mara ya Kwanza tarehe 14.06.2024 baada ya kukamatwa na Jeshi la Polisi na kusomewa shitaka hilo ambapo alikana kutenda kosa hilo.

Upande wa Jamhuri ulileta ushahidi na shauri lilianza kusikilizwa katika mahakama hiyo ambapo mshtakiwa alijitetea na kuomba mahakama imuachie huru akidai ni njama tu zilizotengenezwa na mke wake.

Hata hivyo mahakama baada ya kupitia vifungu vya sheria sambamba na ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamhuri ikiwemo ripoti ya mganga aliyemfanyia uchunguzi mtoto huyo, mahakama imejiridhisha kuwa upande wa Jamhuri wameweza kuthibitisha shtaka hilo bila ya kuacha shaka lolote kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo la kumbaka mjukuu wake na kumhukumu miaka 30 jela ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.