Sotta Mining Sengerema kuanza ujenzi January 2025
19 December 2024, 4:35 pm
Mradi wa uchimbaji mkubwa wa dhahabu uliopo Nyanzaga-Sengerema unatarajiwa kuanza kazi za awali za ujenzi wa mgodi ifikapo Januari, 2025.
Na;Elisha Magege
Wananchi wilayani Sengerema Mkoani Mwanza wametakiwa kuchangamkia fursa mbalimbali zinazokuja kutokana na mgodi wa Sotta Mining Ltd unaotarajia kuanza ujenzi wake mwezi January 2025.
Rai hiyo imetolewa na CPA Elinami Kimaro kutoka tume ya Madini mkoa wa Mwanza alipokutana na madiwani wa Halmashauri ya Sengerema, ambapo amesema viongozi wananpaswa kuwaandaa wananchi kuhusiana na fursa zitakazo patikana kwenye mgodi,ili kuondoa malalamika ya mgodi kuajili watu kutoka mbali na eneo linalozunguka mgodi.
Kwa upande wake meneja mahusiano kampuni ya Sotta Mining Corporation Ltd Bwn. Alen Mpanduji amesema kupitia ziara ya madiwani kufika eneo la mgodi huo litaongeza uwazi na ushirikishaji wa jamii ya wakazi wilaya ya Sengerema kutokana na kuwepo kwa mkanganyiko wa taarifa kuwa tayari mgodi umesha anza kazi.
Mbunge wa Jimbo la Sengerema Mh. Hamis Tabasamu na makamu Mwenyekiti Halmashauri ya Sengerema Makoye Rugata Sengerema wamewataka wananchi kujiandaa na fursa mbalimbali ikiwemo kuanzisha vikundi na kuanza kuzalisha bidhaa zitakazo hitajika mgodini.
Kuanza kwa mgodi wa Dhahabu wa Sotta Mining Ltd unatajwa kuchochea uchumi wa mikoa ya kanda ya Ziwa kwani Zaidi ya ajira 1500 zinatarajia kutolewa kwa watanzania wenye sifa za kufanya kazi eneo hilo.