Jamii yatakiwa kuwapeleka shule watoto wenye ulemavu
12 October 2024, 5:20 pm
Shule ya msingi Tabaruka iliyopo halmashauri ya Sengerema ni miongoni mwa shule zinazofundisha watoto wenye ulemavu Sengerema huku ikikabiliwa na changamoto ya vitendea kazi au vifaa wezeshi kwa watoto hao.
Na Joyce Rollingstone
Shirika lisilokuwa la kiserikali la Sengerema Mshikamano on Disability SMD lililopo wilayani Sengerema mkoani Mwanza, limemkabidhi baiskeli mtoto mwenye ulemavu wa viungo katika shule ya msingi Tabaruka.
Akikabidhi baiskeli hiyo Mkurugenzi wa Shirika hilo Bwn Gervas Titus, amesema kuwa baiskeli hiyo wameitoa kwa ajili ya mtoto Musa Malingo mwenye ulemavu wa viungo, anayesoma katika shule hiyo hatua ya awali.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Bwn Ramadhani Kisinza Joseph, amelipongeza shirika hilo kwa kumsaidia mtoto huyo na kusema kuwa itamsaidia kufika shuleni kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuwaomba waendelee kuwasaidia na wengine wenye mahitaji kama hayo.
Akipokea baiskeli hiyo mzazi wa mtoto huyo Bwn Jemsi Malingo Stephano,amelishukuru Shirika hilo ,huku akiahidi kuitunza na kuhakikisha inatumika kwa matimizi ya mtoto huyo, huku kubainisha changamoto alizokuwa akuzipitia hapo awali.
Naye Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Tabaruka Bwn Dickson Denis, ametoa wito kwa Wazazi na Walezi kuhakikisha mtoto mwenye ulemavu anapata haki zake za msingi ikiwemo Elimu na atakaye kiuka kumpeleka mtoto Shule hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Makabidhiano hayo yamefanyika katika shule ya msingi tabaruka na kuhudhuliwa na walimu,mzazi ,viongozi wa selikari pamoja na viongozi wa shirika la Sengerema Mshikamano On Disability SMD.