Moto wazuka na kuteketeza vitu vya ndani mjini Sengerema
6 October 2024, 5:05 pm
Matukio ya moto kuzuka gafla kwenye nyumba za watu wilayani Sengerema imekuwa ikijitokeza mara kwa mara ambapo jeshi la zimamoto na uokoaji limeendelea kutoa tahadhali kwa wananchi wilayani hapo.
Na;Emmanuel Twimanye
Moto umezuka ghafla na kuteketeza vitu mbambali ikiwemo magunia ya mpunga , vitanda na magodoro katika nyumba ya mkazi mmoja wa mtaa wa Geita Road kata ya Nyatukala Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza,huku chanzo cha moto huo kikiwa bado hakijafahamika .
Akizungumzia tukio hilo Siwema Helman ambaye ni mpangaji wa nyumba hiyo amesema kuwa wakati wakiwa nje ghafla walisikia watoto wakipiga kelele na walipokwenda kuangalia kwenye chumba cha watoto waliona moshi huku Godoro likiteketea kwa moto.
Baadhi ya wananchi wa mtaa huo wamesikitishwa na tukio hilo na kueleza kuwa baada ya kutokea moto huo wameshirikiana na Jeshi la zima moto na uokoaji na kufanikiwa kuzima moto huo .
Mwenyekiti wa mtaa wa Geita Raod Pelana Bagume amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwaomba wananchi kuhakikisha kila mmoja anakuwa na namba za jeshi la zima moto ili yanapotokea majanga ya moto wapate msaada haraka.
Mkuu wa Jeshi la Zima moto na Uokoaji Wilayani Sengerema Juma Ngwembe amewataka wananchi kuwa makini na moto ikiwa ni pamoja na kutowaruhusu watoto kuchezea viberiti ili kuepukana na matukio hayo huku akiwashukuru wananchi waliojitokeza kushiriana na jeshi hilo kuzima moto .