Polisi Sengerema wanolewa uchaguzi serikali za mitaa
27 September 2024, 6:31 pm
Msimamizi wa uchaguzi Halmashauri ya Sengerema ameendelea kutoa elimu ya uchaguzi wa serkali za mitaa kwa makundi mbalimbali katika jamii,uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Nov 27 mwaka huu nchini Tanzania.
Na:Elisha Magege
Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Sengerema Haji Juma amewataka watumishi wa jeshi hilo kuhakikisha wanaelewa vizuri mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 ili kuhakikisha amani na utulivu vinatawala katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi huo.
Ameyasema hayo leo Septemba 27, 2024 wakati wa kikao cha pamoja kilichowakutanisha askari wa jeshi hilo pamoja na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kwa lengo la kutoa elimu ya uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024.
Amesema jeshi la Polisi linao wajibu katika uchaguzi huo, hivyo ni vyema wakaelewa mchakato mzima unavyoenda ili kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani katika kipindi hiki cha kabla na wakati wa uchaguzi.
Sisi jeshi la Polisi kama walinzi wa amani tunao wajibu katika uchaguzi huu, ni lazima huu mchakato tuufahamu vizuri, kuna makosa yanafanywa katika kipindi cha uchaguzi na mwongozo wa kushughulikia makosa hayo upo hivyo ni vyema tuzijue pia tuijue kiomgozo hiyo
Wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kutoka ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri wamewaasa askari wa jeshi la Polisi kuhakikisha wanayajua makosa mbalimbali yanaweza kujitokeza wakati wa uchaguzi kama vile uvunjifu wa amani wakati wa zoezi la kupiga kura, kupiga kura mara mbili, kuharibu orodha ya wapiga kura na makosa mengine yaliyotajwa kwenye mwongozo wa uchaguzi.
Pamoja na hayo askari wa jeshi la polisi pia wamekumbushwa juu ya wajibu wao wakati wa uchaguzi pamoja na matukio mhimu kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa ambao unatarajia kufanyika tarehe 27 Novemba, 2024.